RAIS KIKWETE AMTUMIA SALAMU ZA RAMBIRAMBI MKUU WA MKOA WA SHINYANGA TUKIO LA VIFO VYA WATU 42 HUKO KAHAMA

Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi mkuu wa mkoa wa Shinyanga, Bw. Ali Nasoro Rufunga kuomboleza vifo vya watu 42  huku wengine 91 wakijeruhiwa usiku wa kuamkia tarehe 4 Machi, 2015.

Tukio hilo la kusikitisha limetokea katika kata ya Mwakata iliyoko katika wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga kufuatia mvua kubwa ya mawe iliyonyesha ikiambatana na upepo mkali na kuathiri watu 3,500. 

Katika kata Mwakata iliyoathiriwa zaidi, kaya 350 zimeathiriwa katika kijiji cha Makata wakati katika kijiji cha Nhumbi, kaya 100 zimeathirika. Katika kijiji cha Magung'hwa, kaya 50 zimeathiriwa.


Rais Kikwete amesema msiba huo siyo wa wana-Shinyanga pekee bali ni wa taifa zima ambalo limepoteza nguvu kazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya watanzania kwa ujumla.



Rais Kikwete amewaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao. 

Aidha amewahakikishia wafiwa wote kuwa binafsi yuko pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza msiba huu mkubwa kwao na kwa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527