Ripoti Kamili Picha 14!! SAKATA LA MUUGUZI KUKAMATWA KWA WIZI WA DAWA SHINYANGA,MKUU WA WILAYA AIBUA MAZITO,WAWILI KUSIMAMISHWA KAZI

 

Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro amefanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha afya Kambarage mjini Shinyanga ili kujionea hali halisi jinsi huduma zinavyotolewa kwa wananchi siku moja tu baada ya muuguzi wa kituo hicho kukamatwa kwa tuhuma ya kuiba dawa za serikali.Pichani ni mkuu wa wilaya Josephine Matiro na katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga wakiwa katika chumba cha kuhifadhia dawa wakiwa wamepigwa butwaa baada ya kuona chumba kimesheheni dawa wakati mara kwa mara wananchi wamekuwa wakiambiwa hakuna dawa badala yake wanaambiwa wakanunue kwenye maduka ya watu binafsi mtaani-Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog





Hapa ni ndani ya ofisi ya mganga mkuu/msimamizi wa kituo hicho ambapo mkuu wa wilaya akiwa ameambatana na maafisa wengine wa manispaa ya Shinyanga amekutana na uongozi wa kituo hicho pamoja na wananchi waliomkamata muuguzi mkunga wa kituo hicho Joseph Nkila akituhumiwa kuiba dawa za serikali.Kulia ni Rashid Shaban akimweleza mkuu huyo wa wilaya jinsi walivyofanikisha kufichua wizi huo





Wa pili kutoka kulia ni msimamizi wa kituo cha afya Kambarage Dkt Nassoro Yahya akitoa maelezo kwa mkuu wa wilaya ya Shinyanga kuhusu suala la upungufu wa dawa katika kituo chake ambapo alisema kituo kina upungufu wa dawa na walishatoa taarifa panapohusika siku nyingi zilizopita.Hata hivyo maelezo yake yalipingana na yale ya kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael(mwenye suti pichani) aliyedai kuwa mkoa wa Shinyanga hauna tatizo la upungufu wa dawa bali dawa pekee ambayo haipo ni ile ya Antibiotic




Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akizungumza katika kituo cha afya cha Kambarage mjini Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine amemwagiza mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga kumsimamisha kazi muuguzi Joseph Nkila anayetuhumiwa kuiba dawa za serikali pamoja na msimamizi wa kituo hicho Dkt Nassoro Yahya kwa uzembe unaosababisha mwanya wa upotevu wa dawa katika kituo hicho na kusababisha wananchi kuilalamikia serikali kwa kukosa dawa wakati mkoa wa Shinyanga hauna tatizo la dawa




Mfamasia/mtunza dawa wa kituo cha afya Kambarage Seleman Hamza akitoa maelezo namna anavyofanya kazi katika kituo hicho ambayo hata hivyo mkuu wa wilaya hakuridhika nayo na kumwagiza yeye na msimamizi wa kituo waandae maelezo ya kina ndani ya siku 5




Mmoja wa wasamaria wema waliomkamata muuguzi anayedaiwa kuiba dawa akisimulia jinsi wizi wa dawa unavyofanyika katika kituo hicho na jinsi walivyomkamata Joseph Nkila.Soma hapa Maelezo yake na wenzake



Mkuu wa wilaya Josephine Matiro akiwa katika kituo cha afya Kambarage,nyuma yake ni katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi na kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Sande Deogratius




Dawa zikiwa katika chumba cha kuhifadhia dawa cha Kituo 



Mfamasia/mtunza dawa wa kituo cha afya Kambarage Seleman Hamza akizungumzia kuhusu tukio la wizi wa dawa katika kituo hicho na changamoto ya dawa katika kituo hicho ambapo alisisitiza kuwa kuna baadhi ya dawa hazipo katika kituo hicho




Dawa zikiwa katika chumba cha kuhifadhia dawa kituo cha afya Kambarage 



Dawa katika kituo cha afya Kambarage




Mkuu wa wilaya Josephine Matiro na katibu tawala wa wilaya ya Shinyanga Boniface Chambi wakiwa katika chumba cha kuhifadhia dawa




Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitoka kwenye kituo cha afya Kambarage



Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro akitoa maelekezo kwa kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana Raphael(mwenye suti),kaimu mkurugenzi wa manispaa ya Shinyanga Sande Deogratius na mfamasia wa manispaa ya Shinyanga Emmanuel Zabron



Mkuu wa wilaya Josephine Matiro akimpa maelekezo kaimu mganga mkuu wa manispaa ya Shinyanga Dkt Mhana-Picha zote na Kadama Malunde-Malunde1 blog



********

Hapa Kazi tu ndiyo Tunaweza Kusema!! Novemba 26,2015 asubuhi..Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Josephine Matiro anafanya ziara ya kushtukiza katika kituo cha afya cha Kambarage katika manispaa ya Shinyanga ili kujionea hali halisi ya huduma zinazoendelea katika kituo hicho.

Kubwa zaidi lililomfikisha hapo asubuhi asubuhi ni kuhusu sakata la muuguzi wa kituo hicho Joseph Nkina kukamatwa na wananchi akiwa na dawa za serikali ikiwemo kopo moja la dawa aina ya paracetamol na chupa mbili za dawa ya maji aina ya Erythromycin kinyume na utaratibu.

Baada ya kukutana na uongozi wa kituo hicho na wananchi waliofanikisha kukamatwa kwa muuguzi mkunga wa kituo hicho Joseph Nkila amemwagiza mkurugenzi wa manispaa hiyo kumsimamisha kazi muuguzi huyo kuanzia leo Novemba 26,2015, ili kupisha uchunguzi wa tukio hilo.

“Nimekuja hapa kuona uhalisia wa jambo hili,Kuna ushihidi wa wazi kabisa kuwa muuguzi huyu kweli kaiba dawa za serikali,mbaya zaidi akataka kudanganya kwa kuchukua stakabadhi kutoka kwenye duka la dawa za binadamu (pharmacy), nimekutana na msimamizi wa kituo cha afya Kambarage na mfamasia anayetunza dawa,na kinachoonekana hapa ni uzembe kwenye uongozi kwani dawa zinatoka bila kufuatiliwa kuwa dawa hizo zinafanya nini”,amefafanua Matiro.

“Nitamshangaa sana hakimu atayepindisha kesi hii kwani ushahidi uko wazi kabisa kutoka kwa wananchi kwamba amekuwa akijihusisha na wizi kwa muda mrefu na kumekuwa na malalamiko ya muda mrefu katika kituo hiki cha afya,wananchi wananyimwa dawa,kumbe watu wachache tu wanacheza mchezo huu mchafu wa kuiba dawa”,ameeleza Matiro.

“Kila siku wananchi wanalalamika hakuna dawa,lakini tumeangalia stoo tumekuta dawa zipo za kutosha na Shinyanga hatuna tatizo la dawa,dawa moja tu ambayo ni Antibiotic ndiyo haipo,na tumeagiza iletwe”,alieleza Matiro.

“Cha kusikitisha msimamizi wa kituo hiki Dkt Nassoro Yahya anasema hakuna upotevu wa dawa,huyu naye hatakiwi kuwa hapa kazi imemshinda,nimemwagiza mkurugenzi pia amsimamishe kazi kwani haiwezekani dawa zitoke kwenye kituo bila yeye kufahamu”,amesema Matiro.

Katika hatua nyingine Matiro amewashukuru na kuwapongeza wananchi waliofanikisha kumkamata muuguzi huyo na kuahidi kuwapa zawadi kwa kazi nzuri waliyofanya akiwataka wananchi wengine kuendelea kuwafichua watumishi wasiofanya kazi kwa kuzingatia maadili ya kazi zao

Mkuu huyo wa wilaya ametoa onyo kwa muuguzi aliyekamatwa,ndugu na marafiki kuacha kutoa vitisho kwa wananchi waliokamata dawa hizo na kufanikisha juhudi za kukamatwa kwa muuguzi huyo kinyume na hapo hatua kali za kisheria zitachukulia dhidi yao.

Na Kadama Malunde- Malunde1 blog 
SOMA HAPA HABARI YA JINSI MUUGUZI HUYO ALIVYOKAMATWA 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527