Tanzia_ MBUNGE WA SHINYANGA MJINI 1995 - 2005 LEONARD DEREFA AMEFARIKI BAADA YA KUTOKA KUJISAIDIA NYUMBANI KWAKE




Leonard Derefa enzi za uhai wake

Mwanasiasa mkongwe nchini Tanzania aliyekuwa mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini kupitia CCM mwaka 1995 hadi 2005 Leonard Derefa  amefariki dunia  leo asubuhi kutokana na ugonjwa wa shinikizo la damu muda mfupi baada ya kutoka uwani kujisaidia.

Leonard Derefa( Mwanaderefa) alizaliwa mwaka 1942 katika kijiji cha Bulima wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza na hadi umauti unamfika alikuwa anaishi katika mtaa wa Mbuyuni kata ya Ndembezi katika manispaa ya Shinyanga mkoani Shinyanga.

Mmoja wa watoto wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Newe Derefa amesema baba yake alifikwa na umauti leo saa 12 asubuhi   muda mfupi baada ya kutoka uwani kujisaidia.


Newe amesema kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na mama yake, Thereza Derefa mara baada ya mumewe kutoka uwani aliingia chumbani na badala ya kurejea kitandani alipiga magoti pembezoni mwa kitandani na kuanza kusali huku akitoka jasho jingi mwilini kiasi cha kulowana.

Amesema mama aliamua kumgusa na kumsemesha mume wake ili kujua kitu gani kilichomsibu lakini hakujibu chochote ndipo akatoa taarifa kwake(Newe) juu ya hali ya mzee..

"Kufuatia hali hiyo tulimchukua na kumpeleka katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga, madaktari walimpima ili kuelewa tatizo lakini walibaini tayari  ameishafariki dunia”,amesema Newe.

Kufuatia taarifa za kifo hicho Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Shinyanga kimetoa salaam za rambirambi kwa familia ya marehemu,wanashinyanga, na kueleza jinsi kilivyoguswa na msiba huo  na kwamba marehemu alikuwa mwanachama mwadilifu wa chama na ameacha pengo kubwa kutokana na jinsi alivyokuwa akitegemewa na chama kwa ushauri mbalimbali.

Akizungumza na Malunde1 blog, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga,Khamis Mgeja amesema Mzee Derefa alikuwa mwanachama mchapakazi,mwaminifu, mwadilifu na mshauri mzuri wa chama na jamii kwa ujumla.


“Msiba huu umetugusa sana,kwani mzee Derefa amekuwa kiongozi wa muda mrefu,amekuwa Mbunge,kiongozi wa vyama vya Ushirika,amelitumikia taifa kwa uhodari mkubwa,uaminifu na uadilifu mkubwa kwa ushirikiano mkubwa sana na wenzake”,ameeleza Mgeja.

Jina la Leonard Derefa siyo geni katika ulimwengu wa siasa nchini Tanzania ambapo kwa wafuatiliaji wa masuala ya siasa, hasa tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi, watamkumbuka mwanasiasa huyo mkongwe kutokana na lafudhi yake ya Kisukuma iliyomfanya wakati mwingine apate ugumu kutamka baadhi ya maneno.



Tangu Tanzania ipate uhuru, Jimbo la Shinyanga Mjini limeongozwa na wabunge tisa ambao ni John Rupia, Bakari Msonde, Anna Tito Kachima, Ntemi Nyanda, Haninghton Mfaume, Paul Makune, Leonard Derefa, Dk Charles Mlingwa na sasa Stephen Masele.


Na Kadama Malunde- Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527