NHIF YATOA MAFUNZO JUU YA UHAMASISHAJI KUHUSU UTARATIBU WA UTOAJI MIKOPO YA VIFAA TIBA,UKARABATI WA MAJENGO NA DAWA KWA VITUO VYA AFYA SHINYANGA


Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) leo umetoa semina kwa wadau wa afya mkoani Shinyanga kuhusu Uhamasishaji juu ya Utaratibu wa Utoaji Mikopo ya Vifaa Tiba,Ukarabati wa Majengo na Dawa kwa Vituo vya Kutolea Huduma za Matibabu.Semina hiyo ya siku moja imefanyika katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga huku wawezeshaji wakiwa ni Dkt. Gustav Kisamo ambaye ni afisa mdhibiti Ubora wa Afya kutoka ofisi ya Bima ya Taifa ya Afya mkoa wa Shinyanga(kushoto) na Afisa mkuu Udhibiti Viatarishi Vya Malengo kutoka makao makuu NHIF Thadeus Machume(kulia)-Picha zote na Kadama Malunde-Shinyanga

Mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Ally Rufunga akifungua semina hiyo ambapo alisema katika mwaka wa fedha 2014/2015 NHIF mbali na kuendelea na utoaji mikopo ya vifaa tiba na ukarabati majengo,pia umeanzisha mpango mpya wa utoaji mikopo ya dawa na vitendanishi kwa vituo vyote vya kutolea huduma za matibabu vilivyosajiliwa na mfuko ikiwa ni hatua moja wapo ya kutatua tatizo la upatikanaji wa dawa na vitendanishi katika vituo vya kutolea huduma za matibabu
Afisa mkuu Udhibiti Viatarishi Vya Malengo kutoka makao makuu NHIF Thadeus Machume(Mwezeshaji) akitoa mada kuhusu Uhamasishaji juu ya Utaratibu wa Utoaji Mikopo ya Vifaa Tiba,Ukarabati wa Majengo na Dawa kwa Vituo vya Kutolea Huduma za Matibabu.Alisema NHIF ikiwa na azma ya msingi ya kuboresha huduma za matibabu kwa wanachama wake na watanzania kwa ujumla inatoa mikopo ya vifaa tiba na ukarabati majengo ili kusaidia watoa huduma waliosajiliwa na mfuko waweze kukarabati na kuboresha majengo ya kutolea matibabu na kununua vifaa vya msingi

Afisa mkuu Udhibiti Viatarishi Vya Malengo kutoka makao makuu NHIF Thadeus Machume alisema mikopo inayotolewa na NHIF ni mikopo ya vifaa tiba,mikopo ya ukarabati wa vituo, na mikopo ya dawa na vitendanishi na ili kupata mkopo unachotakiwa ni kufuata taratibu za uombaji mikopo na sio vinginevyo

Wadau wa afya wakifuatilia mada katika ukumbi wa ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga

 Afisa mkuu Udhibiti Viatarishi Vya Malengo kutoka makao makuu NHIF Thadeus Machume akitoa mada.Aliwahamasisha wadau wa afya kufika katika ofisi za NHIF kuomba mkopo kwani ni watu wachache sana wanajitokeza kuchukua mikopo hali inayofanya pesa iendelee kubaki NHIF kutokana na kukosa watumiaji huku vituo vya afya vikiendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa dawa.
Wadau wa afya wakifuatilia kilichokuwa kinajiri ukumbini

Aliyesimama ni Dkt Gustav Kisamo ambaye ni afisa mdhibiti Ubora wa Afya kutoka ofisi ya Bima ya Taifa ya Afya mkoa wa Shinyanga akizungumza katika semina hiyo ambapo alisema dawa ni changamoto kubwa katika vituo vingi vya afya hivyo kuwahamasisha wasimamizi wa vituo vya afya kupata mikopo mbalimbali inayotolewa na NHIF

Afisa mdhibiti Ubora wa Afya kutoka ofisi ya Bima ya Taifa ya Afya mkoa wa Shinyanga Dkt Gustav Kisamo alisema mpango mpya wa utoaji mikopo ya dawa na vitendanishi kwa vituo vyote vya kutolea huduma za matibabu vilivyosajiliwa na NHIF katika awamu ya kwanza utahusisha mikoa 9 ukiwemo mkoa wa Shinyanga

Dkt Daniel Maguja kaimu mganga mkuu mkoa wa Shinyanga akichangia mawili matatu katika semina hiyo

Afisa mkuu Udhibiti Viatarishi Vya Malengo kutoka makao makuu NHIF Thadeus Machume akisisitiza jambo katika semina hiyo

Mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam akizungumza katika semina hiyo ambapo alipongeza mpango mpya wa NHIF kutoa mikopo na kuongeza kuwa halmashauri yake itatoa ushirikiano katika kuhakikisha kuwa vituo vyake vya afya vinapata mikopo ili kuondokana na changamoto zilizopo katika vituo hivyo

Maafisa kutoka NHIF wakifurahia jambo wakati Mstahiki meya wa manispaa ya Shinyanga Gulam Hafeez Mukadam akizungumza  
Kushoto ni katibu tawala msaidizi utawala na utumishi mkoa wa Shinyanga bwana Raymond Kiwesa akizungumza katika semina hiyo ambapo aliwataka wadau wa huduma za afya kutangaza huduma wanazozitoa katika vituo vyao vya afya kwani wananchi wengi wanashindwa kufika kutokana na kukosa taarifa

Waandishi wa habari wakiwa ukumbini
******************
Imeelezwa kuwa bado kuna mwitikio mdogo wa vituo vya afya nchini kuchukua mikopo ya vifaa tiba,ukarabati wa vituo,dawa na vitendanishi kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Hayo yamesemwa leo na Afisa mkuu Udhibiti Viatarishi Vya Malengo kutoka makao makuu NHIF Thadeus Machume wakati wa kikao juu ya Uhamasishaji juu ya Utaratibu wa Utoaji Mikopo ya Vifaa Tiba,Ukarabati wa Majengo na Dawa kwa Vituo vya Kutolea Huduma za Matibabu kilichofanyika katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga.

Alisema  bado mwitikio ni mdogo wa kuchukua mkopo  wadau wanaotoa huduma kupitia mfuko huo jambo ambalo ni changamoto ambayo wanaendelea kuifanyia  kazi.

Alisema tangu kuanzishwa kwa mikopo ya vifaa tiba mwaka 2008 mpaka Desemba 2014 kiasi cha shilingi 10.24 bilioni kiliidhinishwa kwa ajili ya vituo 194 vilivyoomba ni 146 vilikidhi masharti na kuchukua mkopo wa jumla ya shilingi 5.344 bilioni.

Aidha alisema kwa upande wa mikopo ya ukarabati wa vituo vya kutolea huduma mikopo kiasi cha shilingi 6.8 bilioni kiliidhinishwa na iliyokidhi masharti na kuchukuliwa ni shilingi 2.14 bilioni hivyo kuwataka wadau wa afya kujitokeza kuchukua mikopo kwani pesa ipo ya kutosha kwa ajili ya kunusuru vituo vya afya nchini.

“Vituo vingi vya afya vina changamoto ya uhaba wa dawa,vifaa tiba na uchakavu wa majengo,lakini watu wachache sana wanajitokeza kuchukua mikopo,tunaomba sasa mfike kwenye ofisi za bima kwani hakuna mashari magumu wala hauhitaji kutoa rushwa ili kupata mkopo”,alisema Machume.


 Naye afisa mdhibiti Ubora wa Afya kutoka ofisi ya Bima ya Taifa ya Afya mkoa wa Shinyanga Dkt. Gustav Kisamo , aliwashauri wadau hao kutumia mikopo ya vifaa tiba,madawa na vitendanishi sanjari na ukarabati wa majengo ili kuondoa changamoto zilizopo na kuboresha huduma kwa wagonjwa .

“Pesa huwa tunaweka kwenye akaunti za wa kurugenzi wa halamshauri za wilaya lakini tunashauri kila kituo cha afya kiwe na akaunti yake,vituo vya afya vinapaswa kubadilika sasa ili kuwa msaada mkubwa zaidi kwa wananchi”,aliongeza Dkt. Kisamo.

 Kwa upande wake afisa utumishi  mkoa wa Shinyanga Raymond  Kiwesa alisema kutokana na kuwepo kwa changamoto ya upatikanaji wa madawa hivyo mikopo inayotolewa na NHIF itakuwa ni fursa nzuri kwa maslahi ya wananchi.

Katika hatua nyingine alivitaka vituo vya  huduma za afya  kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na watumishi wake kutoa kauli nzuri kwa wateja wao ,hatua ambayo itasaidia kuongeza idadi ya wanachama wa mfuko wa bima ya afya ya Taifa NHIF  sanjari na kuboresha upatikanaji wa madawa na vifaa tiba.

Kwa upande wake kaimu mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt. Daniel  Maguja alionyesha wasiwasi juu ya mikopo inayotolewa kwa kile alichodai kutokuwa na uwazi, huku akiutaka mfuko wa taifa wa bima ya afya kurekebisha mapungufu yaliyopo ili kuongeza idadi ya vituo vitakavyochukua mikopo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post