“CCM ISIPOKUWA MAKINI TUNAIZIKA MWAKA HUU”,ASKOFU HUYU AFUNGUKA,AWAKEMEA WANAODAI KANISA LAKE LIMEJENGWA NA FREEMASONS

Askofu mkuu wa kanisa la KKKT Dayosisi Kusini  Mashariki ya Ziwa Victoria Emmanuel Makala
Askofu mkuu wa kanisa la KKKT Dayosisi Kusini  Mashariki ya Ziwa Victoria Emmanuel Makala amesema Chama Cha Mapinduzi kisipokuwa na umoja mwaka huu kitazikwa.

Askofu Makala aliyasema hayo juzi wakati akiweka wakfu kanda ya Waona Nini kutoka kwaya ya Usharika ya KKKT Ebenezer kanisa kuu Shinyanga iliyozinduliwa katika kanisa hilo ambapo viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wakiongozwa na mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM nchini Mgana Msindai walihudhuria.

Askofu Makala aliwataka wana CCM kudumisha amani ndani ya CCM ili kuendeleza amani iliyopo nchini badala ya kuendeleza malumbano na kwamba isipokuwa makini mwaka huu itazikwa.

 “Nawaasa dumisheni amani ndani ya CCM,dumisheni umoja,muwe kitu kimoja muongoze vizuri,msaidieni rais naye ni mtu mnamtesa,msipokuwa makini CCM tutaizika mwaka huu,kila mtu akitaka kuwa rais hatutafika mbali,hakuna nchi hii haiwezi kuongozwa na marais wawili”,aliongeza Askofu Makala.

“Mimi siyo mwanasiasa lakini tumeapishwa kuwa na sauti za kinabii na kuwaonya watawala kibiblia,kwa hiyo naomba sana kwa amani na ushirikiano tulionao tuendelee kuulinda”,alisema Makala.

Katika hatua nyingine aliwataka viongozi wa siasa kutoona aibu kuingia kwenye nyumba za ibada ili waombewe ili wawe waadilifu badala ya kukimbilia kwa waganga wa kienyeji.

“Nendeni makanisani na misikitini muombewe,kiongozi mzuri ni yule mwenye hofu na mungu,hatutaki kuwa na viongozi wezi na wenye madeni ,msione aibu kuja na hizo pesa mlizonazo msizifiche zileteni kwenye nyumba za ibada hakuna atakayewafukuza”,aliongeza askofu Makala.

Makala alisema ili kuwe na amani nchini lazima watanzania waheshimu mambo ya dini, akisisitiza waislamu na wakristo waachwe waabudu  kwa uhuru na kuacha mambo ya ugomvi wa kidini.

Askofu Makala alisema watanzania wanatakiwa kudumisha umoja na mshikamano walionao na kwamba amani haiwezi kuja kama hakuna uhusiano wa karibu na mwenyeji mungu.

Katika hatua nyingine aliitaka  jamii kuwapuuza baadhi ya watu wanaozusha uvumi kuwa kanisa lake limejengwa kwa nguvu ya Freemasons.

“Kuna watu wanasema kanisa hili limejengwa na Freemason,washindwe walegee kwa jina la yesu,kanisa hili limejengwa na sadaka za wakristo wa kanisa hili na sio vinginevyo”,alisema askofu Makala.

Kwa upande wake mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM nchini Mgana Msindai ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida aliyehudhuria uzinduzi wa albam ya “Waona Nini” alisema Tanzania itaendelea kuwa na amani kutokana na kwamba rais atakayepatikana ameteuliwa na mwenyezi mungu.

“Amani ya nchi hii itaendelea kuwepo kwani kiongozi atakayepatikana ameteuliwa na mungu,sisi tunaamini rais atatokana na mapenzi ya mungu hivyo watanzania wasiwe na wasiwasi wajiandae tu kupiga kura siku ya uchaguzi kwani amani itakuwepo”,alisema Msindai.

Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga Khamis Mgeja aliwaomba viongozi wa dini kuendelea kuiombea nchi ya Tanzania ili amani iendelee kubaki.


“Tanzania ni nchi yetu,sisi pia ni wadau wa amani,tunawaomba viongozi wa dini kuendelea kutuombea na kuliombea taifa kwani amani itaendelea kuwepo kutokana na ushirikiano miongoni mwetu”,alisema Mgeja.

Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527