NAPE NNAUYE AMPONGEZA LOWASSA KWA KUTII AGIZO LA CHAMA


Siku moja baada ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kusitisha makundi yanayokwenda kumshawishi kugombea urais, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, amempongeza kwa kutii agizo la chama hicho.
Nape amesema hatua hiyo ya Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli ni nzuri kwa kuamua kusitisha makundi kwenda kumshawishi agombee urais, ambayo kwa siku chache mfululizo yalikwenda nyumbani kwake Monduli na mjini Dodoma kwa nia hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari jana akiwa katika ziara ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulahman Kinana wilayani Same, Kilimanjaro, Nape alisema anampongeza Lowassa kwa kuwa amekubali kuheshimu kanuni, taratibu na Katiba ya chama ambayo ndiyo inatakiwa kufuatwa na kila mwanachama wa CCM.
Jumanne wiki hii, Nape alimuonya Lowassa kujiepusha na makundi hayo kwa kuwa kufanya hivyo ni kukiuka kanuni na taratibu za chama na kwamba, hali hiyo inamkosesha sifa ya kuteuliwa kugombea urais kupitia CCM.
Nape alisema walimtaka Lowassa, ambaye pia ni mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM azuie makundi yanayokwenda  nyumbani kwake kwa ajili ya kumtaka agombee urais kwani kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati.
“Kilichokuwa kinafanyika ni kuanza kampeni kabla ya wakati na kwa mujibu wa chama chetu ni makosa, maana anakiuka taratibu na kanuni za chama. Hatuwezi kukaa kimya wakati kanuni zinavunjwa wazi, hivyo nimpongeze Lowassa kwa kutii agizo la chama,”  Nape.
Kuhusu shutuma kuwa kauli anazozitoa siyo za chama bali zake binafsi, Nape alisema yeye ndiye msemaji pekee wa chama na hakuna msemaji mwingine, hivyo kauli zinazotolewa ni za chama na siyo zake.
Kanuni na taratibu ambazo nazisimamia zipo miaka mingi kabla ya mimi kuzaliwa. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM nchi nzima niko peke yangu, hivyo lazima nisimamie misingi ya itikadi pamoja na kanuni na katiba ya chama chetu. Kwa nafasi yangu siwezi kukaa kimya wakati kuna watu wanakosea,” Nape.
Akizungumzia kuhusu wapambe wa makada wanaotaka urais, Nape aliwataka kuwa makini wasije wakawaharibia sifa wagombea wao.
Ni vizuri wataka urais wakawa makini na ushauri kutoka kwa wapambe wao kwani wanaweza kuwasababishia kukosa sifa ndani ya chama, nawashauri wote wanaotaka kugombea urais kupitia CCM kutowasikiliza wapambe wao kwa kila wanachoambiwa, maana kuna ushauri mwingine unaweza kuwakosesha sifa za kugombea urais,”  Nape.
Alisisitiza kwamba, kwenye hilo si kwa wapambe wa Lowassa tu, bali ni kwa wapambe wote waliopo nyuma ya makada wanaotaka kugombea urais mwaka huu.
“Ni muhimu kwa makada wote kuhakikisha wanaheshimu kanuni, taratibu na miiko ya chama ili wawe salama, kinyume cha hapo watajipoteza sifa,” alisisitiza Nape.
Zaidi ya vijana 100 wakiwamo wanafunzi wa vyuo vikuu kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara, wamekutana mjini Moshi na kutoa tamko linalodai kwamba, iwapo Lowassa atapoteza sifa za kugombea urais, CCM  kijiandae kisaikolojia kwa sababu kinaweza kupasuka na  kushindwa katika uchaguzi mkuu wa Oktoba.
Vijana hao kutoka Jumuiya za Vyuo Vikuu vya Kanda ya Kaskazini na wengine kutoka sekta binafsi, walitoa angalizo hilo jana mjini Moshi kwa waandishi wa habari, ikiwa ni siku moja tangu Lowassa ajibu kauli ya Nape aliyoitoa Jumanne akidai hawezi kuzuia mafuriko kwa mkono. Via-NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527