ASKOFU GWAJIMA AWASHANGAA POLISI " MANENO NILIYOMPA PENGO NI MANENO YA MUNGU"

 

Kiongozi wa kanisa la Ufufuo na Uzima askofu Joseph Gwajima amefika katika kituo kikuu cha polisi cha jijini Dar es Salaam kwa ajili ya mahojiano na jeshi hilo kwa madai ya kutoa kauli, matusi na maneno makali kwa kiongozi wa kanisa katoliki nchini Muadhama Polycarp Kardinal Pengo.

Kundi la waanmdishi wa habari liliweka kambi katika kituo kikuu cha polisi cha jijini Dar es Salaam kutokana na wito wa jeshi la polisi kupitia vyombo vya habari kumtaka kiongozi huyo wa kanisa la ufufuo na uzima kufika kituoni hapo kwa mahojiano kwa madai ya maneno ya kashfa na matusi kwa kiongozi wa kanisa katoliki nchini.

 Kutokana na adha ya foleni kubwa ya magari katika jiji la Dar es Salaam ilibidi kushuka katika gari lake na kutembea kwa miguu akiwa na walinzi wake kutoka katikati ya jiji hadi kituo kikuu cha polisi.

Mara baada ya kuwasili katika kituo hicho alipokelewa kwa mahojiano ya awali kutoka kwa vyombo vya habari ambapo askofu Gwajima amesema maneno aliyoyatoa ni ya kumkemea kiongozi mwenzake wa kiroho kwa madai ya kukiuka msimamo wa viongozi wengine wa dini wa kuikataa mahakama ya kadhi.

Akijibu swali kuhusu sababu za kufanya hivyo badala ya kutumia maneno ya kistaarabu askofu Gwajima amedai kuwa maneno aliyoyatoa ni maneno ya mungu huku akishangazwa na wito wa polisi kwa kuwa maneno hayo hakuyatoa kwa jeshi la polisi bali kwa kiongozi mwenzie wa kiroho.

Hivi karibuni katika mitandao ya kijamii kumezagaa picha za video zikiambatana na maneno ya kashfa kwenda kwa kiongozi wa kanisa katoliki nchini Muadhama Polycarp Kardinal Pengo jambo lililofanya jeshi la polisi kumtaka kufika kituo kikuu cha polisi kwa mahojiano zaidi.
Via>>ITV

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527