UMEZIONA PICHA DKT MAGUFULI WAKATI AKIONGOZA JARIBIO LA SAFARI YA KIVUKO CHA MV DAR ES SALAAM? ZIKO HAPA



Kivuko cha Mv Dar es Salaam, kinachotarajiwa kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria kutoka Dar es Salaam kwenda Bagamoyo, jana kilifanyiwa majaribio ya safari ambapo kilitumia saa tatu, huku ikielezwa kwamba kitakapoanza kutoa huduma kitatumia saa mbili kwa safari moja.

Akizungumza katika ziara ya ukaguzi wa Kivuko hicho, Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, alisema wamekifanyia majaribio ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mwisho.
 
Baada ya majaribio hayo kwa mujibu wa Dk Magufuli, wanatarajia ndani ya siku 15 watakuwa wamekamilisha taratibu zote, ambapo kitazinduliwa na Rais Jakaya Kikwete kwa ajili ya kuanza huduma.
 
Alisema kivuko hicho kilichotengenezwa na kampuni ya Johs Gram Hansen ya Denmark, kitakuwa na vituo saba hadi kufika Bagamoyo na kinatarajiwa kupunguza msongamano mkubwa na adha ya usafiri kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.
 
Vituo hivyo kwa mujibu wa taarifa za Wizara hiyo ni Magogoni, Kawe, Jangwani Beach, Rungwe Oceanic, Mbweni, Kaole na Mbegani.
 
Aidha Dk Magufuli alisema watahakikisha wanaendelea kuwapa kazi Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Kamandi ya Maji, kutokana na utendaji wao mzuri hasa katika ukarabati wa vivuko na ujenzi wa gati.
 
"Nawahakikishieni kwamba tutaendelea kuwapa kazi Jeshi kutokana na utendaji wenu, ingawa najua maneno haya yanaweza yasiwafurahishe Wakala wa Ufundi na Umene(Temesa), ila ukweli ndiyo huo," alisema.
 
Aidha aliwahakikisha wananchi wa kigamboni kwamba usafiri utaendelea kuimarika, ambapo pia imetengwa Sh bilioni tatu katika bajeti, kwa ajili ya ununuzi wa kivuko kingine huku ujenzi wa daraja ukiendelea.
 
"Tutaendelea kuimarisha usafiri wa majini ili kupunguza msongamano na foleni katika barabara... Tunawashukuru sana wananchi kwa kuendelea kuvumilia matatizo madogo madogo ya usafiri, nawaahidi tutaendelea kutoa ushirikiano, ili kuhakikisha matatizo hayo yanaisha,"alisema.
 
Dk Magufuli alisema kivuko hicho kina vifaa vya kisasa, ikiwemo uwezo wa kuona jiwe au mlima hata wakati wa usiku na kina mwendo wa kasi.
 
Kuhusu nauli, Dk Magufuli alisema kitakapoanza kutoa huduma, watapanga nauli nafuu ambayo kila mwananchi ataimudu, ili atakayetumia kivuko hicho aone nafuu kuliko kupanda daladala.
 
Naye Mtendaji Mkuu wa Temesa, Marycelina Magesa, alisema kivuko hicho kimetengenezwa kwa fedha za Serikali kwa asilimia 100 na kimegharimu Sh bilioni 7.9 na kinauwezo wa kubeba abiria 300.
 
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Raymond Mushi alisema kivuko hicho kitasaidia kuinua shughuli za wananchi wa mkoa huo na Pwani kwa kupunguza foleni, ambazo zimekuwa zikipoteza muda mwingi barabarani.
 
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo alisema kivuko hicho kimekuja muda muafaka hasa katika Mkoa huo, kwa kuwa Bagamoyo ni eneo la Ukanda wa Kiuchumi na utakuwa mji wa uwekezaji mkubwa kuanzia Julai mwaka huu.
 
Aidha aliomba Wizara hiyo kuboresha miundombinu hasa upande wa Bagamoyo, ili iwe rahisi kwa wananchi kwa kuwa kwa sasa hali watalazimika kupanda magari mawili ili kufika kwenye kivuko.
 
"Naomba miundombinu iboreshwe na pawe na usafiri wa moja kwa moja hadi mjini kwa sababu kwa sasa mtu akitoka mjini, analazimika kushuka Zinga ndiyo aje hapa Mbegani kupanda kivuko ila ukiwepo usafiri wa moja kwa moja utasaidia sana," alisema.
 
Katika ziara hiyo, Magufuli alisafiri hadi Bagamoyo na viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo kutoka wizara hiyo, Temesa, Wakala wa Barabara (Tanroad), JWTZ Kamandi ya Maji na wananchi ambao walipata fursa ya kwenda Bagamoyo na kurudi bila malipo.




~Mpekuzihuru

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527