HII HAPA HOTUBA YA HAKIMU WA SHINYANGA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA NCHINI TANZANIA LEO



Hakimu mkazi mwandamizi mfawidhi wa mahakama ya mkoa wa Shinyanga John Chaba  akizugumza leo wakati wa maadhimisho ya siku ya sheria nchini,ambapo kimkoa yamefanyika katika viwanja vya mahakama ya hakimu mkazi Shinyanga leo asubuhi-picha na Kadama Malunde
Ifuatayo ni hotuba iliyotolewa na hakimu huyo

Mhe. Mkuu wa Wilaya (ambaye kimsingi unamwakilisha Mkuu wa (M) wetu wa Shy)
Mhe. Hakimu Mkazi Mfawidhi (W) Shinyanga,
Wahe. Mahakimu wa ngazi zote,
Mhe. Wakili wa Serikali Mfawidhi, Shinyanga,
Mhe. Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Kujitegemea Tawi la (M) Shinyanga,
Wahe. Mawakili wote wa Serikali na Mawakili Binafsi/Kujitegemea,
Mhe. Mtendaji wa Mahakama (M) wa Shinyanga,
Wahe. Makamanda wa vyombo vya Ulinzi, Magereza, na Usalama wa Mkoa,
Wahe. Viongozi wa Dini kutoka Mathehebu mbalimbali,
Wahe: Viongozi na Wakuu wa Taasisi za Serikali mliopo, Mashirika ya Umma, na Viongozi wote wa Vyama vya Siasa,
Watumishi wote wa Mahakama wa ngazi zote mliopo hapa,
Wageni waalikwa, Mabibi na Mabwana.  (Itifaki imezingatiwa)



Bwana Yesu asifiwe, Tumsifu Yesu Kristo, Asalaam Aleikhum,








UTANGULIZI
Mhe. Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa, kwa heshima kubwa kabisa naomba nianze kwa kuwatakia Kheri ya Mwaka Mpya – 2015.

Pili, naomba nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kutupa afya njema na rehema kuiona siku hii njema. Lakini pia, naomba nikushukuru sana wewe Mhe. Mgeni Rasmi na Wote mlioalikwa kwa kukubali mwaliko wetu ili kujumuika nasi kwenye maadhimisho haya ya siku ya Sheria hapa Nchini (Law Day) ambayo kimsingi huadhimishwa kila mwaka. Hakika ni furaha kubwa kuwa pamoja nanyi katika kuadhimisha na kusherehekea maadhimisho haya kama wadau muhimu wa chombo hiki cha Mahakama.

Aidha, natambua na kuthamini kazi na majukumu mazito mliyonayo katika jamii yetu na Taifa kwa ujumla. Hata hivyo, siku hii njema mmeipa umuhimu wa pekee na kuonyesha ishara ya upendo, mshikamano, ushirikiano na udugu kama watanzania wamoja na wenye nia moja ya kulijenga Taifa lenye nguvu. Hali hii inaonyesha kwamba hakika mnathamini na kutambua vema kazi na wajibu wa chombo hiki katika jamii yetu.
  
Mhe. Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa, leo hii sisi tuko hapa Mkoani Shinyanga, na kuna wenzetu ambao wako maeneo mengine Nchini kote wakiadhimisha siku hii muhimu na adhimu. Kama tunavyofahamu, siku hii ya Sheria Nchini ni siku ambayo inaashiria mwanzo rasmi wa Kalenda ya kuanza kwa shughuli za Mahakama Nchi nzima. Kwa kawaida, siku hii hutumika kuwaombea dua pamoja na sala watumishi wote wa Mahakama hususani watendaji wakuu wakiwemo Wahe. Majaji na Mahakimu ili waweze kufanya kazi zao katika misingi ya haki, lakini zaidi wakimtumainia Mungu kwa kuwa tunaamini kwamba watendaji hawa kwa ujumla wanahitaji kuwa na hofu ya Mwenyezi-Mungu ili waweze kufanya kazi zao za utendaji wa haki kwa wananchi na Taifa kwa ujumla kwa mujibu wa Sheria.

Kwa niaba ya Mahakama ya Mkoa – Shinyanga, napenda kuwaalika tena leo hii katika maadhimisho haya na kuwashukuruni nyote kwa kufika kwenu, hususani viongozi wetu wa dini ambao kimsingi wamefanya kazi kubwa kutuombea sisi watendaji na watumishi wengine ili tuendelee kuwa na afya njema, hekima, busara na uwezo tupate kutekeleza majukumu yetu kwa mujibu wa kanuni, taratibu na Sheria za Nchi.

 

MADHUMUNI

Mhe. Mgeni Rasmi na Wageni waalikwa, siku hii ya leo ni siku muhimu sana kwetu sote. Umuhimu wake haupo tu kwa Mahakama pekee bali hata kwa wadau wa Mahakama kwa ujumla. Kwa pamoja tunapata wasaa mzuri wa kukumbushana wajibu wetu na pia kujikosoa na kukubali kukosolewa lakini tukiwa na dhamira moja tu ya kuhakikisha kwamba tunafanya kazi kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za Nchi. Kwa wale wenye uelewa wa sheria mtakubaliana na mimi kuwa moja ya msingi mkuu wa haki unasema - sio tu kwamba haki itendeke, lakini ionekane kuwa imetendeka.

Mhe. Mgeni Rasmi, kama ilivyo ada, Siku ya Sheria Nchini huadhimishwa ikiwa na kauli mbiu. Kwa mwaka huu, kauli mbiu inasema; FURSA YA KUPATA HAKI : WAJIBU WA SERIKALI, MAHAKAMA NA WADAU”.

Mhe. Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa, naomba nijadili kauli mbiu hii kwa ufupi. Unapoisoma kauli mbiu ya mwaka huu kuna mambo mawili muhimu yanayohitaji kujadiliwa. Mambo haya nimeyaweka katika mfumo wa maswali ili niweze kueleweka vizuri. Moja, tunaposema fursa ya kupata haki hii ina maana gani katika mchakato mzima wa utoaji haki hapa Nchini? na lingine ni nini wajibu wa Serikali, Mahakama na Wadau kwa ujumla katika mchakato huu wa utoaji haki?.
 

I.           MAANA YA NENO HAKI
Kimsingi neno Haki lina maana pana na halina tafsiri ya moja kwa moja.  Kwa tafsiri ya Kikamusi, kwa mujibu wa kamusi ya Oxford neno haki (Justice) linatafsiriwa kuwa ni “hali ya usawa na busara” (The guality of being fair and reasonable). 

Pia, Kamusi ya Black’s Law imetafsiri neno haki kuwa ni “Kulinda ukweli na kuadhibu mabaya kwa kutumia usawa”, yaani “Protecting Rights and punishing wrongs using fairness)  

Na kwa upande, Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) kwenye moja ya repoti yake ya tarehe 09/03/2004 imetafsiri dhana hii ya Fursa ya Kupata haki kuwa ni sehemu ya uzima au uhai wa Shirika hili la Maendeleo la Umoja wa Mataifa ambalo limepewa mamlaka ya kupunguza/kushusha kiwango cha umaskini na kukuza utawala wa Kidemokrasia miongoni mwa jamii ya Kimataifa.


I.            FURSA YA KUPATA HAKI.
Mhe. Mgeni Rasmi na Wageni waalikwa, fursa yakupata Haki ni dhana pana ambayo msingi wake ni uwezo wa watu kutafuta na kupata haki stahiki kutoka Taasisi rasmi na zisizo rasmi za utoaji haki kwa kuzingatia usawa na vigezo vya haki za Binadamu. Fursa hii ya kupata haki inaweza kuelezewa vizuri zaidi kwa mtazamo wa wazo la kisiasa lijulikanalo kama egalitariarism ikiwa na maana ya believing in or based on the principle that all people are equal and deserve aqual rights and opportunities (kwa lugha ya kitaalamu). Dhana hii, ni mfululizo wa falsafa ya kisiasa unaolenga usawa wa mtu mmoja mmoja. Kila mtu anapaswa kuwa sawa na mwengine, aangaliwe sawa, au kwa uwiano ulio sawa. Kwa mafano, Katiba ya Nchi na Sheria nyingine zieleze wazi kuwa msimamo wa utawala wa sheria usiwe tu katika kusimamia haki za msingi kwa wananchi, bali iwe kwa ajili ya kusimamia usawa na heshima kwa watu wote. Falsafa hii inapigania zaidi uwepo wa usawa wa thamani ya mtu pamoja na utu wake. Ni dhana inayofungamana na mfumo wa kisiasa na kijamii na kimsingi dhana hii inashadidia zaidi ufanisi wa upatikanaji wa haki uliojikita katika misingi ya usawa.

Kwa ustaarabu huo, fursa ya kupata haki haitazami/kuangalia tofauti za kiuchumi au kijamii zilizopo kati ya mtu na mtu. Dhana iliyo sawa na hii imerithiwa na Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosimamia, mbali na mambo mengine, upatikanaji wa haki. Hili limebainishwa wazi na Ibara ya 13 ya Katiba; ambayo inasema:-

Watu wote ni sawa mbele ya sheria, na wanayo haki, bila ya ubaguzi wowote kulindwa na kupata haki sawa mbele ya sheria

Mhe. Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa, tujikumbushe kidogo kauli iliyotolewa na Wah. Majaji wa Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, JJ.A Omar, Ramadan na Mnzavas iliyotolewa katika kesi ya Clay Laway Vs. Republic[1] (1992) CA T.L.R. 72 walisema:-

All individuals should be free and equal in considering that every person is entitled to recognition and respect of his dignity, therefore they entitle equality before the law without any discrimination towards access to justice and right to life in particular.”  
Mhe. Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa, Kama ilivyobainishwa na Mahakama ya Rufaa, fursa ya kupata haki inamuwezesha kila mmoja wetu kuitumia sheria kwa minajili ya kulinda haki zetu. Hata hivyo, hili litawezekana pale tu vyombo vya umma pamoja na mfumo wa utoaji haki na taasisi husika utapohakikisha kuwa kila mtu analindwa na sheria na anauwezo wa kuufikia mfumo waa utoaji haki. Tukiwa tumejumuika hapa, tunapaswa kukumbuka kuwa, miongoni mwa mambo yanayoleta usawa katika nchi ni fursa sawa ya kupata haki (rights), uwepo wa uhuru wa mtu binafsi, na fursa ya kupata haki yenyewe (justice). Tukumbuke kwamba, dhana hii ya fursa ya kupata haki imejikita katika sifa kuu moja, kwamba hawa watunga sheria pamoja na maafisa wa juu wa Serikali wawe watenda haki (fair and just) katika mchakato mzima wa utoaji/upatikanaji wa haki kwa watu wote.

Kwa maana hiyo, ikitokea kuwepo kwa ukiritimba, ugumu au ukaidi wa makusudi wa kutotenda haki, Mahakama ndicho chombo pekee kilichopewa mamlaka ya juu ya kusimamia haki ya kila mmoja wetu. Wakati Ibara ya 107A ya Katiba inasema:

“Mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa ni Mahakama”.

Ibara ya 13 (3) ya Katiba yenyewe inasema:-
“Haki za raia, wajibu na maslahi ya kila mtu na jumuiya ya watu yatalindwa na kuamuliwa na Mahakama na vyombo vinginevyo vya Mamlaka ya Nchi vilivyowekwa na sheria au kwa mujibu wa sheria”.

Hii ina-maana kwamba Mahakama kama chombo pekee chenye mamlaka ya mwisho ya utoaji haki hapa Nchini, endapo haki inayotafutwa katika vyombo vingine vya Kisheria itashindikana kupatikana, jibu lake ni Mahakama zetu. Hata hivyo, tunaweza kusema, iwapo fursa ya kupata haki itatolewa katika Taasisi zote za Serikali na zisizo za Serikali pamoja na wadau wengine kwa ufasaha, Mahakama zetu hazitakuwa na mlundikano wa maashauri au kesi kutokana na migogoro mbalimbali katika jamii yetu.

Mhe. Mgeni rasmi na Wageni waalikwa, sambamba na yale niliyoyasema hapo awali, kuna mahusiano ya moja kwa moja kati ya uelewa, kuwa na habari muhimu ama ufahamu wa namna ambavyo Mahakama inafanya shughuli zake kwa ujumla. Kimsingi, wananchi wanayohaki ya kufahamu shughuli za Mahakama siyo tu katika kutafsiri sheria na kutoa haki, bali pia kutambua sheria husika ambazo mara nyingi hutumika Mahakamani. Kwa mfano; Wananchi wanahaki ya kujua sheria za Makosa ya Jinai na Madai, migogoro ya ardhi, Mambo ya Mirathi, Sheria za Uchaguzi, Sheria za Mazingira, Sheria zinazohusu mali-asili (nishati na madini, utalii), vyombo vya habari, n.k.

Hata hivyo, haitoshi kwa huyu mwananchi kuwa na uelewa, kupata habari muhimu na kufahamu namna ambavyo Mahakama inafanya shughuli zake kwa ujumla. Kubwa zaidi ni kwa mwananchi huyu kuipata fursa ya kupata haki yake, na kwa upande wa pili, ni namna gani Serikali, Mahakama yenyewe na Wadau kwa ujumla wanawajibika ipasavyo kuhakikisha kwamba mwananchi huyu anapata fursa hii kwa mujibu wa sheria na bila kikwazo chochote. Napenda kutumia fursa hii kuwaomba na kuwakumbusha wale wote ambao tumepewa dhamana ya kushughulikia upatikanaji na utoaji wa haki kwa wananchi tunatimiza wajibu wetu ipasavyo.  

Kwa maoni yangu, ili ufahamu huu umfikie mwananchi hatuna budi kushirikiana kwa pamoja kuwaelimisha wananchi na jamiii kwa ujumla kuitumia fursa hii ya kupata haki katika vyombo vinavyohusika  kama moja ya hatua za msingi katika kuufikia mfumo wa utoaji haki na utatuzi wa migogoro katika jamii yetu kwa ujumla.

Pamoja na ukweli kuwa Mahakama ndicho chombo pekee chenye mamlaka ya kutoa haki kwa wananchi, kwa upande mwingine, Serikali na Wadau wote wa Mahakama wameendelea kuwa kiungo na sehemu muhimu siyo tu katika kuhakikisha fursa ya kupata haki inafikiwa, lakini pia, wamekuwa na wajibu wa kuhakikisha kwamba fursa hii inafikiwa tena kwa wakati.  Hii ina-maana kwamba endapo chombo kimoja kitashindwa kutekeleza wajibu wake ipasavyo inaweza kuwa kikwazo kwa fursa hiyo kufikiwa kwenye chombo kingine, jambo ambalo kwa maoni yangu ni hatari na linaweza kupelekea haki kuchelewa kupatikana ama kutopatikana kabisa.  Tukumbuke kwamba ufanisi wa chombo kimoja cha utoaji wa haki unategemea sana utendaji wa chombo kingine katika mchakato mzima wa utoaji haki hapa nchini. 


II.        WAJIBU WA SERIKALI, MAHAKAMA NA WADAU

Mhe. Mgeni rasmi na Wageni Waalikwa, baada ya kuzungumzia kwa kifupi kuhusu dhana hii ya Fursa ya kupata haki katika mchakato mzima wa utoaji haki hapa nchini, sasa naomba nizungumzie kipengele cha pili kama nilivyokwisha dokeza hapo juu. Nini wajibu wa Serikali, Mahakama na Wadau wa Mahakama kwa ujumla katika mchakato huu wa utoaji haki?.

Mhe. Mgeni Rasmi na Wageni Waalikwa, hapa nchini fursa ya kupata haki imeendelea kuwa ni ndoto na jambo gumu kuifikia hususani kwa jamii ambazo ziko pembezoni/jijini na masikini kwa ujumla katika jamii yetu, japo sasa taratibu imeaanza kuonekana kwa kuwa Serikali na wadau wake wa maendeleo wameunganisha nguvu zao kwa kuweka mazingira ambayo yanaruhusu huduma za kisheria kuwafikia wananchi waalioko chini - down to the grassroots level. Pamoja na juhudi za muda mrefu za Serikali yetu kuhakikisha kwamba wananchi wanapata fursa ya kupata haki zinaonekana kuzaa matunda, lakini uhalisia wa mambo ni kwamba fursa hii ya kupata haki haijazaa matunda kwa namna inayofaa hususani miongoni mwa jamii inayoishi pembezoni. Mara kadhaa tumesikia habari za kutisha na kusikitisha zinazoambatana na uvunjaji wa haki za binadamu.
                                                         
Ili mwananchi apate fursa ya kuufikia mfumo wa utoaji haki hapa nchini kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu tulizonazo, lazima Serikali kwa upande wake, Mahakama na Wadau wenyewe watimize wajibu wao.

Mhe. Mgeni Rasmi naomba nitaje kwa kifupi baadhi ya mambo ambayo ni wajibu wa Serikali, Mahakama na Wadau.


Ø  WAJIBU WA SERIKALI
(i) Kuhakikisha vyombo vya Serikali vinashirikiana na kutimiza majukumu yake ipasavyo.

Katika kuhakikisha fursa ya kupata haki inafikiwa vyombo vya Polisi, Magereza, Takukuru, Ofisi ya Waendesha mashitaka / Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Ustawi wa Jamii, Takukuru n.k, vina wajibu mkubwa katika kuhakikisha fursa ya kupata haki inafikiwa.  Kwa mfano ili mshitakiwa afikishwe Mahakamani ni lazima Polisi ama Takukuru wakamilishe upelelezi wao kikamilifu na ndipo wanasheria wa Serikali wanaweza kuendelea na shitaka husika na hatimaye kuipa Mahakama fursa ya kusikiliza na kutoa uamuzi.  Na endapo chombo kimoja kitashindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu basi fursa ya kupata haki haiwezi kufikiwa.  Serikali inawajibu wa kuhakikisha vyombo hivi vinatengewa bajeti pamoja na vitendea kazi vya kutosha ili vitimize majukumu yake kikamilifu.

          (ii) Kukuza na kuhamasisha ufahamu wa sheria.

Mhe. Mgeni rasmi na Wageni Waalikwa, ili jamii iweze kuwa na fursa ya kupata haki inatakiwa kuwa na uelewa wa kutosha juu ya haki na wajibu wao na namna ya kudai haki hizo.  Serikali inawajibu wa kuhakikisha inawahamasisha na kuwawezesha wananchi kuwa na elimu ya ufahamu juu ya Sheria za Nchi kupitia vyombo vya habari, vipeperushi, Makongamano, Mikutano ya hadhara, Kampeni mbalimbali, n.k

(c) Kujenga na kuboresha miundo mbinu ya Mahakama, Polisi, Magereza na kuajiri watumishi wa kutosha wanaokidhi vigezo nya utumishi wa umma.

Katika kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kupata haki, suala la miundo mbinu ya Mahakama kwa maana ya majengo, Vituo vya Polisi, Magereza pamoja na upanuzi wa magereza ni jambo la msingi na muhimu.  Suala la kuwa na idadi ya watumishi wanaokidhi vigezo na mahitaji kama vile Majaji na Mahakimu, watumishi wengine wa Mahakama, Askari polisi, Askari Magereza, na Wanasheria wa Serikali kwa ujumla ni jambo ambalo Serikali lazima ilitazame kwa jicho la pekee kwa kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa inajenga imani kwa jamii tunayoihudumia. Hakika kukosekana kwa huduma za Kimahakama au vituo vya polisi na uhaba wa watumishi hii inaweza kupelekea wananchi kukosa fursa ya kupata haki au kusafiri umbali mrefu kuipata. Serikali inawajibu wa kuhakikisha inaboresha majengo na kuajiri watumishi wa kutosha.



Ø  WAJIBU WA MAHAKAMA

Mhe. Mgeni na Wageni waalikwa, imani na sifa ya wananchi kwa mahakama haviwezi kujengwa na kudumishwa kama wananchi hawajui jinsi Mahakama inavyofanya kazi zake. Wananchi hawana budi kupewa nafasi ya kuelewa vyema umuhimu wa chombo hiki cha Mahakama katika mchakato mzima wa utoaji haki nchini na uhuru wake kwa ujumla. Pamoja na mambo mengine, chombo hiki kina wajibu wa:

(i)                 Kutenda haki kwa wote na kwa wakati.

Mahakama kama chombo pekee na kilele cha utoaji haki, ina-wajibu wa kuhakikisha kwamba wananchi wanakifikia chombo hiki bila kikwazo na inatoa maamuzi kwa wakati na ufanisi kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa. Ibara ya 107A (2) inasema;

“Katika kutoa uamuzi wa mashauri ya Madai na Jinai kwa kuzingatia Sheria Mahakama zitafuata Kanuni zifuatazo, yaani;

(a)   kutenda haki kwa wote bila ya kujali hali ya mtu kijamii au kiuchumi,
(b)   Kutochelewesha haki bila sababu ya msingi,
(c)    …..
(d)   …..
(e)    …..

Mhe. Mgeni rasmi, Wananchi hawawezi kukiona chombo hiki cha Mahakama kama kimbilio la kutatua migogoro yao ikiwa tu maamuzi ya Mahakama hayatakuwa ya haki na kutolewa kwa wakati. Badala yake wananchi hawa wanaweza kuwa wanajichukulia sheria mkononi kwa sababu tu yakukosa imani na chombo hiki.
(ii)               Kusimamia maadili ya watumishi wa Mahakama.

Suala la kutoa haki linatawaliwa na uaminifu na uadilifu wa hali ya juu kwa Jaji au Hakimu pamoja na watumishi wa Mahakama. Tunaweza kuwa na Sheria nzuri lakini kama watendaji hawa na watumishi kwa ujumla watakosa uaminifu na uadilifu, hakika haki haiwezi kutendeka na wananchi wanaweza kupoteza imani na chombo hiki na hata kushindwa kwenda Mahakamani kutafuta haki zao kwa hofu ya kutotendewa haki. Kwa maana hiyo, Mahakama inawajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa watumishi wote katika ngazi zote wanazingatia maadili ya utumishi wa Umma.

Mhe, Mgeni rasmi na Wageni Waalikwa, kwa kutambua umuhimu wa suala la maadili, Mahakama ya Tanzania hivi sasa ipo katika mageuzi mbalimbali ambayo yanalenga katika kuboresha huduma ya utoaji haki nchini. Mageuzi hayo ni pamoja na Mabadiliko ya Sheria Na. 4 ya Mwaka 2011 ya Uendeshaji wa Mahakama, lengo kuu likiwa ni kurahisisha huduma ya utoaji haki ikiwa ni pamoja na kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu. Kutokana na mageuzi haya, hivi sasa kuna Watendaji wa Mahakama katika kila mkoa, ambapo hatua hii pia imelenga katika kuhakikisha  kuwa majukumu ya kiutawala yanatekelezeka na Watawala na pia yale ya Kimahakama yanatekelezwa na Wasajili na Mahakimu na hatimaye kurahisisha huduma ya upatikanaji wa haki kwa wakati.

Mhe, Mgeni rasmi na ageni Waalikwa, pamoja na ukweli kwamba hali ya majengo ya Mahakama tunazofanyia kazi mengi ni chakavu na pengine hayafai kwa ajili ya shughuli za Kimahakama, ni vema sisi watendaji na watumishi kwa ujumla tutambue kwamba Uongozi wa juu wa Mahakama ya Tanzania umejipanga kuboresha majengo yake, ikiwa ni pamoja na kujenga upya na kukarabati majengo yenye unafuu. Kupitia maadhimisho haya, napenda kutoa rai kwa watumishi wenzangu katika Mkoa wa Shinyanga na wengine kote Nchini, kufanya kazi kwa bidii ili kujenga imani kwa wananchi tunaowahudumia. Ninaamini, kama kila mtumishi wa Mahakama atafanya kazi yake kwa uaminifu na uadilifu itakuwa rahisi kwa wananchi siyo tu kwenda/kufika  Mahakamani kudai haki zao, lakini pia, Mahakama itakuwa na uwezo wa kushughulikia kesi husika na kufanya maamuzi ya haki.

Tukumbuke kwamba kuelimisha jamii juu ya haki na wajibu wao kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu tulizonazo inachangia kwa kiasi kikubwa kuleta mwamko kwa jamii kufika katika vyombo vya kutoa haki kudai haki zao.

Ø  WAJIBU WA WADAU WA MAHAKAMA

Wadau wa Mahakama ni kundi ambalo linajumuisha wananchi wenye kesi Mahakamani (wadaawa), Polisi, Magereza, Ofisi ya Waendesha Mashtaka, Mawakili wa kujitegemea, Taasisi za Serikali na zisizo za Kiserikali, Madalali wa Mahakama, Takukuru, Ustawi wa Jamii, Mashirika ya Umma, N.G.O’s, Asasi za Kiserikali na Kiraia, n.k. Kundi hili lina wajibu wa kuelemisha jamii kujua haki zao na namna ya kuufikia mfumo wa utoaji haki pamoja na kutoa msaada wa kisheria. Kundi hili linawajibu mkubwa wa kuhakikisha wananchi wanaelimishwa kiasi cha kutosha juu ya haki zao na sheria za nchi.  Pia ni wajibu wa kundi hili kutoa msaada wa kisheria kwa gharama ya chini ili kuwapa wananchi unafuu wa kupata huduma za kisheria.  Kufanya hivyo, kundi hili lina nafasi kubwa ya kuisaidia jamii kuwa na uwezo wa kuutumia mfumo wa utoaji haki kikamilifu.  Maeneo ya pembezoni mwa nchi yetu hasa vijijini watu wamekuwa hawapati fursa ya kupata haki kwa sababu tu hawana uelewa wa kutosha juu ya haki zao, mbali na kutofahamu sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo. Tatizo la kiuchumi na fedha nalo limechangia kwa kiasi kikubwa kuwafanya wananchi kukosa haki zao.    Aidha, Asasi za Kiraia zina wajibu mkubwa wa kutoa elimu ya msaada wa kisheria pamoja na kuwawezesha au kuwapa uwezo wa Kisheria (Legal empowerment) kwa madhumuni ya kuwa na ufahamu na kutambua namna ya kutafuta na hatimaye kupata fursa ya kupata haki zao.



(iv)             HALI HALISI YA FURSA YA KUPATA HAKI KATIKA MKOA WETU WA SHINYANGA

Mhe. Mgeni na Wageni waalikwa, naomba pia niseme japo kwa ufupi kuhusu hali halisi ya fursa ya kupata haki katika Mkoa wetu wa Shinyanga. Katika Mkoa wetu wa Shinyanga fursa ya kupata haki inakabiliwa na changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto hizi ni pamoja na:-

1.   UCHAKAVU WA MIUNDO MBINU YA MAHAKAMA
Kuna uhaba mkubwa wa Majengo ya Mahakama na mazingira yasiyo rafiki ya kufanyia kazi hususani kwa watumishi wa Mahakama zilizo pembezoni.  Kwa ujumla, suala hili limekuwa ni kikwazo kwa wananchi kuweza kupata fursa ya kupata haki. Hii inatokana na ukweli kuwa watumishi wengi wa Mahakama wamekuwa wakiacha kazi au kufanya kazi katika mazingira magumu.  Matokeo yake Mahakama nyingi zina kosa Mahakimu na kupelekea wananchi kushindwa kupata fursa ya kupata haki.

2.   RUSHWA
Kama tunavyofahamu, rushwa ni adui wa haki, na rushwa ni kikwazo cha fursa ya kupata haki katika maeneo yetu ya kazi.  Tafiti mbalimbali za hivi karibuni zinautaja mhimili wa Mahakama kuwa ni wa pili baada ya jeshi la polisi kwa ulaji wa rushwa. Mtaalam mmoja aitwae Bryan A. Stevenson ambaye ni Profesa katika Chuo Kikuu Cha New York, Shule ya Sheria ambae pia ni mwanzilishi na Mkurugenzi wa Taasisi ya Haki sawa huko Marekani, aliwahi kusema, na nina mnukuu;
          
Mfumo wetu utakuhudumia vizuri kama ni tajiri na mwenye hatia, kuliko ukiwa masikini na usiwe na hatia.”  Mwisho wa  Kunukuu.

Na aliyewahi kuwa Rais wa 11 Inchini India (kati ya Mwaka 2002 - 2007) Bw. A.P.J. Abdul Kalam aliwahi kusema maneno haya; na nina-mnukuu;

 Kama nchi inataka kuondokana / kutokuwa na rushwa na kuwa nchi yenye fikira njema, kwa dhati ninafikiri kuna watu  watatu katika jamii yetu wanaweza kupelekea kuwa tofuati ambao ni Baba, Mama na Mwalimu.”  Mwisho wa Kunukuu.

Mhe. Mgeni rasmi na wageni waalikwa, wale wanaofanya kazi za kimahakama watakubaliana na mimi kwamba rushwa ni kitendo kinachoondoa uhuru wa maamuzi ya kuzingatia misingi ya haki.  Rushwa siyo tu imekuwa kikwazo katika kuhakikisha haki inatendeka, lakini pia, imekuwa ni kikwazo kwa wananchi kuufikia mfumo wa utoaji haki kwa hofu kuwa hawataipata au kutendewa haki.  Mbali na watendaji wa Mahakama kwa maana ya Majaji na Mahakimu,  kumekuwepo na wimbi kubwa la watumishi wengine wa mahakama wasio waadilifu na wasio wa watumishi wa Mahakama kudai kupewa rushwa na wengine kudiriki kutumia majina ya Majaji na Mahakimu kuomba rushwa.  Nichukue fursa hii kuwataka watumishi wote wa Mahakama katika Mkoa wetu wa Shinyanga  na Taifa kwa ujumla kuzingatia maadili ya utumishi wa Umma na ninaiomba Serikali na Jamii kuwa mstari wa mbele kukemea rushwa kuanzia ngazi ya familia.

3.   ELIMU JUU YA HAKI, WAJIBU NA SHERIA KWA WANANCHI
Katika Mkoa wetu wa Shinyanga, sehemu kubwa ya wananchi waishio vijijini (pembezoni) wamekuwa na uelewa mdogo kuhusu suala zima la haki zao na wajibu walionao kwa chombo hiki cha Mahakama. Lakini, kwa maeneo ya mijini kwa kiasi kikubwa yameendelea kunufaika na fursa hii ya kupata habari na kuwa uelewa juu ya haki zao kupitia vyombo vya habari na Wanahabari wenyewe, Mikutano ya hadhara, Mafunzo maalumu, Vipeperushi, Mbao za Matangazo, Taasisi za kutoa misaada na ushauri wa kisheria, tofuati na maeneo ya vijijini ambako fursa hii haipatikani kwa urahisi. Changamoto hii imepelekea wananchi walio wengi kushindwa kuufikia mfumo wa utoaji haki kwa kwa sababu ya mazingira waliyonayo. 

Napenda kutoa rai kwako wewe Mhe. Mgeni Rasmi, viongozi wote mliopo hapa, hususani viongozi wa Halmashauri zetu, Asasi za Kisheria, Wanahabari, viongozi wetu wa vyama vya siasa, na wote mnaonisikiliza kwa pamoja tushirikiane kutoa elimu na kuielimisha jamii pamoja na kuiwezesha kuipa elimu ya Kisheria juu ya haki zao na wajibu wao kwa chombo hiki cha Mahakama kwani kwa namna moja ama nyingine, hii inaweza kuwa ndiyo tiba na suluhu ya changamoto hii. Baba wa Taifa aliwahi kusema, Inawezekana, Timiza wajibu wako.




MWISHO
Mhe. Mgeni rasmi na Wageni waalikwa, katika kuhitimisha salamu zangu, napenda kumalizia kwa kusema kwamba ili fursa ya kupata haki iweze kufikiwa, ni lazima vikwazo kama vikwazo vya kiuchumi, lugha, elimu juu ya haki na Sheria, n.k. vinaondolewa.  Kwa upande wake, Serikali, Mahakama, na Wadau wa Mahakama wanawajibu mkubwa wa kushirikiana kwa pamoja sambamba na wadau wengine wa maendeleo katika nyanja ya sheria katika utoaji wa elimu, huduma na misaada ya kisheria bila malipo kwa jamii ambayo inakipato cha chini kwa maana ya paralegals and pro bono publico kuhakikisha vikwazo hivyo vinaondolewa na wananchi wanapata fursa ya kupata haki zao kwa wakati. Lakini pia natoa rai kwa watumishi wenzangu kujipanga vizuri kwa ajili ya kutekeleza majumu ambayo yako mbele yetu na hasa tukizingatia kwamba maadhimisho haya yanaashiria mwanzo rasmi wa shughuli za Kimahakama, huku tukijiandaa kwa ajili ya uzinduzi rasmi wa jengo letu la Mahakama kuu Shinyanga.





Baada ya kusema hayo napenda kuwashukuruni nyote kwa usikivu wenu.

Asanteni Sana na Mungu awabariki.



 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527