Imeelezwa kuwa magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo mkoani Shinyanga ni pamoja na Malaria,Ukimwi,kisukari na shinikizo la damu huku ajali ya pikipiki nazo zikichangia kwa hali nyingine vifo vya watu wengi mkoani Shinyanga.
Hayo yamebainishwa juzi na mganga mkuu wa mkoa wa Shinyanga Dkt
Ntuli Kapologwe wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
Dkt Kapologwe alisema ugonjwa malaria ni tishio mkoani
Shinyanga na ndiyo ugonjwa ambao unaua watu wengi hususani watoto wengi wenye
umri chini ya siku 28 na wengine chini ya miaka mitano.
Alisema katika kipindi cha mwezi Januari hadi Desemba watoto
98 wenye umri chini ya siku 28 walipoteza
maisha kutokana ugonjwa wa malaria.
Dkt Kapologwe alisema ugonjwa wa UKIMWI pia bado ni tishio
mkoani Shinyanga na kwamba watu wengi wakiwemo watoto,vijana na wazee
wanaendelea kupoteza maisha kutokana na ugonjwa huo hivyo kuitaka jamii kuepuka
mara moja sababu zinachochangia kuambukizwa virusi vya Ukimwi kwa taifa
linapoteza nguvu kazi kila kukicha.
Magonjwa mengine yanayosababisha vifo vingi mkoani humo ni
ugonjwa wa kisukari na shinikizo la damu,ambapo hivi sasa yanawapata zaidi
vijana tofauti na zamani ambapo magonjwa hayo yalikuwa yanadaiwa kuwapata watu
wenye umri mkubwa(wazee).
Mganga huyo mkuu wa mkoa wa Shinyanga alisema mbali na
magonjwa hayo manne,ajali za barabarani hususani za pikipiki zinachangia kwa
kiasi kikubwa vifo vya wananchi wa mkoa huo.
Alisema takwimu zinaonesha kuwa hospitali ya mkoa wa
Shinyanga pekee kila siku inapokea mgonjwa mmoja aliyepata ajali ya pikipiki
hivyo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari wanapoendesha vyombo vya moto
barabarani.
Katika hatua nyingine aliwataka wakazi wa Shinyanga kufika
katika vituo vya afya,zahanati na
hospitali ili kupata huduma kwani dawa zote muhimu zinapatikana kwa asilimia 98
na watoa huduma wana ujuzi na weledi wa hali juu katika kuhudumia wagonjwa.
“Tumepeleka dawa za kutosha kwenye vituo vyote vya
afya,zahanati na hospitali zote,Shinyanga hatuna tatizo la upungufu wa
dawa,malalamiko yaliyopo sasa ni wagonjwa kulalamikia baadhi ya wauguzi
kuwatolea lugha mbaya”,alieleza Dkt Kapologwe.
Na Kadama Malunde-Shinyanga