Tumefika Pabaya Shinyanga!! ASKARI WA FFU APIGWA JIWE KWA KOMBEO,ANG'OLEWA MENO 6,ANGALIA PICHA HAPA

Pc Idd  Makame(25) aliyejeruhiwa vibaya mdomoni kwa kung’olewa meno sita baada ya kupigwa jiwe kwa kutumia kombeo na watu wanaodaiwa kuwa ni wachimbaji haramu wa madini katika mgodi wa Mwadui akiwa amelazwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga

Pc Idd  Makame(25) akiwa wodini


MFANO WA SILAHA(KOMBEO) ILIYOTUMIKA KUMJERUHI PC IDD- Pichani ni mkulima katika kijiji cha Mwamala kata ya Mwamashele katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga akitumia kombeo maarufu kwa jina la Nh’ago kufukuza ndege aina ya Kwelea kwelea kwenye shamba la mtama-Picha kutoka Maktaba ya Malunde1 blog.

Kumetokea tukio la aina yake katika mgodi wa madini ya almasi wa Mwadui uliopo katika wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga ambapo askari polisi wa kikosi cha kutuliza ghasia kutoka jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Pc Idd  Makame(25) amejeruhiwa vibaya mdomoni kwa kung’olewa meno sita baada ya kupigwa jiwe kwa kutumia kombeo (kwa lugha ya Kisukuma Nh'ago) na watu wanaodaiwa kuwa ni wachimbaji haramu wa madini katika mgodi wa Mwadui wakati akitimiza wajibu wake wa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao

Tukio hilo la kusikitisha limetokea Novemba 21,2014 saa mbili na robo usiku katika eneo la Tanex katika mgodi huo wakati askari huyo akiwa na askari wenzake wakiongeza nguvu baada ya askari wa kampuni ya ulinzi ya Zenneth iinayolinda mgodi wa Mwadui kushindwa kuwadhibiti wachimbaji wadogo wa madini maarufu "Wabeshi" waliotaka kuingia kwa nguvu mgodini wakiwa na silaha za jadi.

Mashuhuda wa tukio hilo wameiambia Malunde1 blog kuwa  kampuni ya ulinzi ya Zenneth Security Services Limited inayolinda mgodi huo ilipata taarifa kuwa kuna wachimbaji haramu maarufu kwa jina la Wabeshi waliotaka kuvamia mgodi huku wakiwa na silaha za jadi ikiwemo mishale,mikuki,virungu,makombeo,mapanga na fimbo.

Kufuatia hali hiyo askari hao wa Zenneth wakifika eneo la tukio kuwadhibiti Wabeshi hao lakini ghafla walianza kushambuliwa kwa silaha za jadi.

Baada ya kuona wanazidiwa nguvu,askari wa Zenneth walilazimika kuomba msaada wa askari wa kikosi cha kutuliza ghasia (FFU) cha jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga.

Baada ya askari wa FFU kufika eneo la tukio nao walianza kushambuliwa na Wabeshi hao ,ndipo PC Idd akapigwa jiwe mdomoni kwa kutumia kombeo na kung’oka meno sita mdomoni na kukimbizwa katika hospitali ya mkoa wa Shinyanga kwa ajili ya matibabu.

Mkurugenzi wa kampuni ya ulinzi ya Zenneth Security Services Limited Elisha Ndulu amethibitisha uwepo wa tukio hilo.

Naye mganga mfawidhi wa hospitali ya mkoa wa Shinyanga Dkt Mfaume Salum amesema Pc Idd alipigwa na kitu chenye ubapa mdomoni na kusababisha meno sita kung’oka na anaendelea kupatiwa matibabu,hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Justus Kamugisha alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuongeza kuwa tayari wanawashikilia watu wanne kwa mahojiano zaidi na wanaendelea kufanya uchunguzi ili kuwakamata wahusika wengine.
Na Kadama Malunde-Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527