YULE "MTOTO WA MIUJIZA" AELEZA UCHAWI WAKE


 
Mtoto Happiness (10) anayeishangaza jamii kwa matukio ya kimazingara. 

mtoto Happiness (10) aliyetikisa kwa tukio la kupanda ndege kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Zanzibar bila kujulikana limeibuka tena, safari hii katika sura mpya kufuatia mtoto huyo kufungua kinywa chake na kuanika mambo ya kichawi, Uwazi lina mkanda mzima.

Mtoto huyo aliyaanika mambo hayo mwishoni mwa wiki iliyopita mbele ya Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar, SACP Mary Nzuki na kumfanya afande huyo kupigwa butwaa. 

Aidha, alizungumza na mwandishi wa habari hizi, nyumbani kwao, Mkuranga.

ALICHOSEMA AWALI NI HIKI

Awali akizungumza kwa kujiamini, mtoto huyo ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Mkokozi Kata ya Vikindu wilayani Mkuranga, Pwani, alikiri kusafiri kwa ndege hadi Zanzibar akidai alikwenda kumfuata baba yake mzazi aishiye huko.

Hata hivyo, mama yake mzazi, Sarah Zefania alimpinga mwanaye huyo na kusema: “Baba yake haishi Zanzibar, yupo Kipunguni (Ilala jijini Dar es Salaam).”

 
Mtoto Happiness akiwa na mama yake 

KUHUSU UCHAWI
Mtoto Happiness alikwenda mbele zaidi kwa kujiongeza akisema katika maisha yake amekuwa akifanya mambo ya kishirikina lakini si peke yake. 

Alisema ana mshirika wake (hakumtaja jina).
Happiness aliutaja ushirikina huo. Alisema amekuwa akisafiri usiku mara kwa mara na mshirika wake huyo wa karibu kwa kutumia usafiri wa ungo!!

ATAJA PAKA, NYOKA NA MBUZI
Kama vile haitoshi, mtoto huyo ambaye ametokea kushangaza wengi huku akipachikwa majina ya ‘mtoto wa ndege’, ‘mtoto wa uchawi’ na ‘mtoto wa miujiza’, alisema akiwa katika safari hizo amekuwa akiwaona paka, nyoka na mbuzi.

AFIKA POPOTE BILA KUJALI UMBALI
Aliongeza kuwa, kwa kutumia ungo na huyo mshirika wake, wamekuwa na uwezo wa kufika popote wanapopataka bila kujali umbali.

 
Mkoba ukiwa na nguo za Mtoto Happiness

 MAVAZI YA SAFARINI
Akizidi kufunguka, Happiness alisema mara nyingi wanapokuwa katika safari hizo ambazo alisema watu hawawezi kuwaona, huvaaa nguo nyeupe, nyeusi au wakati mwingine nguo nyekundu ili kufanikisha masuala yake ya usiri.

Mtoto huyo aliyasema hayo kufuatia Septemba 16, mwaka huu kudakwa tena maeneo ya Feri jijini Dar akiwa na begi ambapo alisema anamfuata baba yake (hakusema wapi).

Baada ya walinzi wa eneo hilo kumgundua ni ‘mtoto wa ndege’ walimfikisha Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar ambapo mama yake aliitwa.

Mama alishtuka baada ya kumwona mwanaye akiwa amebeba begi lililokuwa na nguo kwa madai ya kuwa alikuwa akielekea kwa baba yake mzazi.

 
Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, Dar, SACP Mary Nzuki 
SIKU YA KUTOROKA MARA YA PILI

Akisimulia kisa cha kutoroka mara hii ya pili, Happines alisema siku ya tukio mtu mmoja ambaye alidai kuwa ni kaka yake wa kambo alifika nyumbani na kumchukuwa yeye na begi lake la nguo akidai anampeleka kwa baba yake Zanzibar lakini baada ya kufika Feri mtu huyo alitokomea kusikojulikana.

KAULI YA MAMA
Wakati mama huyo (pichani) akizungumza na wanahabari wetu alimtaka baba wa mtoto huyo, Julius kujitokeza ili kunusuru hatima mbaya ya mtoto wao.

WACHUNGAJI WANENA
Waandishi wetu waliwatafuta baadhi ya wachungaji wa makanisa ya kiroho nchini ili wazungumzie tukio la mtoto huyo.

 
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zakary Kakobe.

 NI MAPEPO
Mchungaji wa Kanisa la Paradise International la jijini Dar, Gideon Parapanda alisema tatizo linalomsumbua mtoto huyo ni pepo mchafu wa kuzimu hivyo kwa kutumia maombi ndani ya makanisa hali hiyo itatoweka.

“Happiness kama alizaliwa salama na hali hiyo imemkuta ukubwani na kufanya mambo ambayo hayaeleweki ni pepo wachafu ambapo akimtumainia Yesu tatizo hilo litaisha mara moja,” alisema Mchungaji Parapanda.

WAZAZI WASIENDE KWA WAGANGA

Naye Mchungaji wa Kanisa la Cathedral of Joy, pia ni Nabii John Komanya, yeye alisema Happiness anasumbuliwa na pepo wachafu, kitu pekee ni maombi na alitahadharisha wazazi au ndugu wasiende kwa waganga wa kienyeji.

ASKOFU KAKOBE ATAKA APELEKWE FULL GOSPEL
Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zakary Kakobe yeye alisema matatizo ya Happiness yataisha kwa Jina la Yesu kama ndugu, walezi au wazazi wataamua kumfikisha kanisani kwake.

“Kinachomsumbua mtoto huyo ni roho chafu, akiombewa katika makanisa ya kiroho atafunguliwa, hata kama ndugu wakiamua kumleta hapa Full Gospel ni sawa tu, atakombolewa,” alisema Kakobe.


BONYEZA HAYA MANENO TUKUTUMIE HABARI ZETU MARA TU ZINAPOTOKEA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527