UCHAGUZI CHADEMA WAFUNGULIWA KWA KUCHAPANA MAKONDE HUKO GEITA,MWENYEKITI APIGWA MAWE


UCHAGUZI wa viongozi wa chama na mabaraza ya(CHADEMA)katika kata ya Kalangalala mjini Geita uliokuwa unafuatiliwa na malunde blog kuanzia asubuhi juzi ulitanguliwa na vurugu kubwa zilizopelekea mwenyekiti wa Mtaa wa Tambukaleli kupitia chama hicho kujeruhiwa vibaya mdomoni na mgongoni.

Tukio hilo lilitokea majira ya saa 6:46 mchana muda mfupi baada ya wasimamizi wa uchaguzi huo kutoka kanda ya ziwa magharibi kuwasili eneo la uchaguzi huo amabo awali ulitakiwa kufanyikia kwenye ukumbi wa ofisi ya serikali ya mtaa wa Mkoani inayoongozwa na Chadema.

Mapema asubuhi kabla ya ugeni huo kuwasili eneo hilo hali ya usalama na utulivu ilikuwa imetanda huku wanachama wa chama hicho wakiwa wamekaa makundi wakibadilishana mawazo na kila mmoja akiwa na shauku ya uchaguzi huo.

Hata hivyo katika hali isiyokuwa ya kawaida katibu wa mwenyekiti wa mtaa huo wa Mkoani,Peter Donald(CHADEMA)alifika eneo hilo kisha kufunga ukumbi uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya mkutano wa uchaguzi akidai kufanya hivyo kutokana na maagizo aliyopewa kutoka juu kisha kuondoka eneo hilo akiwaacha wanachama wa chama hicho wakiwa wameduwaa.

Majira ya saa 6:23 wasimamizi kutoka kanda waliwasili eneo hilo wakiwa na gari namba T 156 CDA aina ya Ranger Ford na kuelezwa kuwa ukumbi wa chama chao uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya kikao ulikuwa umefungwa kwa maelekezo ya aliyekuwa katibu wa jimbo hilo kabla ya kuvuliwa madaraka Rogers Luhega akishirikiana na mwenyekiti wa mtaa huo Peter Donald ambaye pia ni diwani ya kata hiyo kupitia chama chao.

Wakati ugeni huo ukipata maelezo hayo lilitokea kundi la wanachama wa chama hicho linalomuunga mkono Luhega kisha kuvuruga maongezi hayo na kuanza kuporomosha matusi ya nguoni kwa wasimamizi hao kutoka kanda na kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwemo Daud Ntinonu aliyedhalilishwa kwa kila aina ya matusi lakini hakujibu lolote.

Kundi hilo lililokuwa likiongozwa na baadhi ya viongozi wa Chadema akiwemo Neema Stephen Chozaile(Mratibu Bavicha Mkoa wa Geita),Elikana Gidion(Katibu mwenezi tawi la Nyanza),Peter Mazura(bodigadi wa kujitegemea wa Luhega),Sospiter Sweya(Mwenyekiti tawi la mwatulole)
Tom Revons(Katibu tawi shilabela),Fikiri Charles Toi(Mwenyekiti kata ya kalangalala aliyejihudhuru)na Albert Machumu pamoja na mambo mengine lilijiapiza kuwa liko tayari kupoteza maisha lakini si kushuhudia uchaguzi huo unafanyika.

Wakati hayo yakiendelea wasimamizi wa uchaguzi huo walikuwa kimya wasijue la kufanya na baada ya muda kundi hilo lilibeba mawe na kuanza kuwashambulia wenzao na moja likatua mdomoni na mgongoni kwa mwenyekiti wa mtaa wa Tambukaleli Mabula Ndoshi aliyejeruhiwa vibaya.

Kufuatia hali hiyo baadhi ya wanachama walitimua mbiyo huku dereva wa gari lililokuwa limebeba wasimamizi hao akitumia uzoefu wake kwa kuwabeba viongozi hao kisha kuliondosha kwa kasi gari hilo ambalo liliokolewa na Redbrigade wa chama hicho waliofika eneo hilo mara moja kisha kuwadhibiti kundi lililoleta vurugu ambalo nalo lilitimua mbio kukwepa mkong’oto kutoka kwa vijana hao wa ulinzi wa chadema.

Vurugu hizo zilitulia majira ya saa 7:40 na msamalia mmoja wa eneo hilo alitoa ukumbi na uchaguzi ukaendelea kwa amani ambapo hata hivyo baada ya kura kupigwa uongozi wote wa kata hiyo chama na mabaraza uliokuwa umefutwa kimizengwe na aliyekuwa katibu wa chama hicho jimbo la Geita,Luhega ulichaguliwa kwa mara nyingine tena.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mara baada ya uchaguzi huo,Neema Mafula(Msimamizi mkuu wa Uchaguzi huo) na Elikana Paschal waliwatoa wasiwasi viongozi waliochaguliwa pamoja na wanachama wa chama hicho kuhusu vurugu zinazoendelea ndani ya chama hicho na kuahidi kulifikisha suala hilo uongozi wa juu ili walitolee uamuzi.

Siku moja kabla ya uchaguzi huo aliyekuwa  katibu wa chama cha demokrasia na maendeleo(CHADEMA),jimbo la Geita,kabla ya kuvuliwa wadhifa huo na kamati kuu ya Chadema Taifa Rogers Luhega na anayedaiwa kuwa kambi ya mbunge wa kigoma kaskazini Zitto Kabwe aliapa kuzuia huo uchaguzi wa kata na wa jimbo usifanyike mbali na maagizo hayo kutoka kamati kuu Taifa ya Chadema iliyoagiza uchaguzi huo ufanyike ndani ya wiki hii.

Uchaguzi huo alioapa kuuzuia  usifanyike mbali na kuwa ni agizo kutoka kamati kuu ya chadema Taifa aliufuta hivi karibuni kwa maslahi yake binafsi.

Na Victor Bariety-Malunde1 blog-Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527