Baadhi ya waandishi wa habari wakimsikiliza Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Frederick Werema wakati wa mkutano uliofanyika leo jijini Dar es Salaam.
Viongozi wa vyama vya siasa waliopo nje ya Bunge Maalumu la Katiba wameaswa kurejea bungeni ili kufanya maridhiano ndani ya bunge hilo.
Kauli hiyo imetolewa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alipokuwa akiongea na waandishi wa habari leo Jijini Dar es salaam.
Jaji Werema amesema kuwa wajumbe walio nje ya Bunge Maalum hawana budi kurejea bungeni na kuacha kumshinikiza Rais kulivunja bunge hilo kwani hana mamlaka ya kulivunja kulingana na sheria inayoliongoza bunge hilo.
“Sheria inasema kuwa baada ya bunge hilo linaweza kuvujwa baada ya katiba kupatikana, kinyume na hapo bunge husitishwa kufikia maridhiano na kufikia mwafaka kwa kufuata misingi ya demokrasia.” alisema Jaji Werema.
Pia Jaji Werema alisema kuwa wajumbe walio nje ya bunge hilo hawana budi kurudi ili kuendelea kujadili vipengele vingine vya rasimu ili kuweza kupata katiba iliyo bora kwa nchi na watu wake.
Aidha, Jaji Werema aliviasa vyombo habari kutumia nafasi yao ya kuwa mhimili muhimu katika uongozaji wa nchi kutokuwa na upendeleo katika utoaji wa taarifa na kuacha kuongozwa na mawazo ya wachache ili kuweza kusaidia nchi kupata Katiba Mpya kwa manufaa na maendeleo ya nchi.
Na Rose Masaka-MAELEZO
Social Plugin