TAZAMA PICHA- WAREMBO (WASHIRIKI) SHINDANO LA MISS SHINYANGA 2014 WATOA MSAADA WA CHAKULA KITUO CHA WATOTO WENYE ULEMAVU CHA BUHANGIJA MJINI SHINYANGA


Hapa ni katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Buhangija katika manispaa ya Shinyanga ambapo leo Warembo 20 wanaoshiriki shindano la kutafuta mrembo wa mkoa wa Shinyanga(Miss Shinyanga 2014) wakiongozwa na mwandaaji wa Mashindano hayo bi Asela Magaka wa Asela Promotions   wametembelea kituo  na kutoa msaada wa vyakula huku wakichangia kidogo walichokuwa nacho kwenye mifuko yao kuchangia ujenzi wa bweni katika kituo hicho chenye watoto zaidi ya 260.Pichani ni baadhi ya warembo wakiwa na baadhi ya watoto wenye ulemavu wa ngozi wakionesha upendo

Watoto wenye ulemavu waoishi katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Buhangija mjini Shinyanga wakiwa na baadhi ya washiriki wa shindano la Miss Shinyanga 2014
Warembo hao 20 wametembelea kituo hicho cha kulelea watoto wenye ulemavu wa ngozi,wasioona na wasiosikia ikiwa ni katika maandalizi yao ya shindano la kutafuta mrembo wa mkoa wa Shinyanga(Miss Shinyanga 2014) litakalofanyika Juni 28,214 mjini Kahama,ambapo Mzee Yusuph akiwa amembatana na wasanii wengine kibao watatoa burudani siku hiyo,Katika hali ya pekee shindano hilo litatanguliwa na shindano la kutafuta mrembo mwenye kipaji mkoa wa Shinyanga(Miss Talent Shinyanga) kesho Juni 25,2014 katika ukumbi wa NSSF mjini Shinyanga ambapo mwimbaji wa taarabu Isha Mashauzi atakuwa akitoa burudani

Misaada iliyotolewa na Asela Promotions na  kukabidhiwa kwa mkuu wa  kitengo cha Walemavu katika kituo cha Buhangija Jumuishi mwalimu  Bright Mduma ni pamoja na,chumvi katoni 1, mchele kilo 100,unga wa sembe kilo 200,sukari kilo 20,mafuta ya kupikia lita 10,unga wa ngano kilo 50 na sabuni za unga za kufulia kilo 30, vyote vikiwa na thamani ya shilingi 506,700/=.

Watoto wenye ulemavu wakiwa katika eneo la tukio leo

Aliyesimama ni mkuu wa  kitengo cha Walemavu katika kituo cha Buhangija Jumuishi mwalimu  Bright Mduma akizungumza wakati wa kupokea msaada wa chakula kutoka Asela Promotions,ambapo alisema miongoni mwa changamoto zilizopo katika kituo hicho ni upungufu wa mabweni ambapo watoto wanalazimika kulala zaidi ya mmoja kitanda kimoja.Kulia ni mwandaaji wa Shindano la Miss Shinyanga na Miss Talent Shinyanga 2014 bi Asela Magaka  akiwa ameshika tama baada ya kupewa taarifa kuhusu hali ngumu ya maisha wanayoishi watoto wenye ulemavu

Aliyesimama Mkuu wa kitengo cha Walemavu kituo cha Buhangija mwalimu Bright Mduma aliwashukuru washiriki wa shindano la Miss Shinyanga kwa kuona umuhimu wa kufika katika kituo hicho ili kuona hali halisi ya maisha ya watoto wenye ulemavu katika kituo cha Buhangija Jumuishi mjini Shinyanga

Aliyesimama ni mwandaaji wa Mashindano ya Miss Shinyanga mwaka 2014 bi Asela Magaka kutoka Asela Promotions,ambaye amekuwa akifanya maandalizi ya Mamiss Tangu mwaka 1999 akizungumza leo katika kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Buhangija mjini Shinyanga.Magaka alisema ameamua kuwapeleka warembo hao katika kituo hicho ili kujua mambo yanaoendelea katika jamii ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni “Urembo, sanaa na jamii” hivyo ni vyema wakajua kuwa urembo unahusiano na mambo ya jamii,wajue jamii inahitaji nini,na umuhimu wa kusaidia jamii,hii itasaidia warembo hawa kuwa mabalozi wazuri katika kusaidia watu mbalimbali  wenye mahitaji maalum katika jamii.

Kushoto ni mlezi wa warembo(Matron) bi Asha saidi

Aliyesimama ni bwana Mustapha Ramadhani ambaye ni mwalimu wa Mamiss kanda ya ziwa akizungumza katika kituo cha Buhangija ambapo kufuatia changamoto ya mabweni aliahidi kuchangia mfuko 1 wa saruji kwa kuungana na Warembo 20 wanaoshiriki wa shindano la Miss Shinyanga 2014 kuchangia mifuko 18 ya saruji kwa ajili ya  kuchangia ujenzi wa bweni la wavulana lililoanza kujengwa 2013 na Miss Tanzania mwaka 2012 Brigette Alfred.

Baada ya kufika katika kituo hicho cha kulelea watoto wenye ulemavu,baadhi ya washiriki wa shindano la Miss Shinyanga 2014 walijikuta wakitokwa na machozi na kuiomba serikali kuwachukulia sheria mara moja watu wanaohusika na mauaji ya albino na kuitaka jamii kubadilika na kuacha dhana ya kwamba watapata utajiri kupitia viungo vya albino

Bwana Shaban ambaye pia ni mwalimu wa Mamiss kanda ya ziwa akizungumza mawili matatu katika kituo cha watoto wenye ulemavu wa ngozi,wasioona na wasiosikia cha Buhangija mjini Shinyanga.Pamoja na mambo mengine aliahidi kutoa kilo 20 za ngano kwa ajili ya watoto hao

Baadhi ya washiriki Miss Shinyanga 2014-Kushoto ni bi Nyangi Warioba kutoka Msalala kulia ni bi Mary Emmanuel kutoka Ushetu ambao waliguswa na maisha ya watoto wenye ulemavu na kusababisha watokwe na machozi na kuamua kuchangia mifuko miwili ya saruji kuchangia ujenzi wa bweni lililoanza kujengwa na Miss Tanzani mwaka 2012 Brigette Alfred.Warembo wote 20 wameahidi kuchangia mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi huo ikiwa ni kukamilisha mifuko 18 ya saruji

Kushoto ni mwandaaji wa shindano la Miss Shinyanga 2014 bi Asela Magaka kutoka Asela Promotions akikabidhi vyakula(moja ya mifuko ya unga wa sembe) kwa mkuu wa  kitengo cha Walemavu katika kituo cha Buhangija Jumuishi mwalimu  Bright Mduma

Katikati ni Yasinta kwa niaba ya watoto wenye ulemavu wa  katika kituo cha Buhangija akipokea unga wa sembe 

Mwakilishi wa watoto wenye ulemavu Yasinta akizungumza kwa niaba ya watoto wenzake baada ya kupokea zawadi ya chakula kutoka kwa washiriki wa shindano la Miss Shinyanga wakiongozwa na Asela Promotions ambapo aliwapongeza kwa kitendo hicho na kuongeza kuwa  hivi sasa wanayo changamoto ya upungufu wa Shuka na magodoro

Mmoja wa washiriki wa shindano la Miss Shinyanga 2014 bi Nicole Sarakikya kutoka Kishapu akiwa na watoto wenye ulemavu wakifuatilia kilichokuwa kinajiri-Picha zote na Kadama Malunde-Shinyanga

Habari kamili soma hapa chini
 Zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya kufanyika shindano la kutafuta Mrembo wa mkoa wa Shinyanga,leo warembo 20 wanaoshiriki shindano hilo wakiongozwa na mwandaaji wa Mashindano hayo bi Asela Magaka (Asela Promotions) wametembelea kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu cha Buhangija katika manispaa ya Shinyanga na kutoa msaada wa vyakula sambamba na kuchangia mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa bweni katika kituo hicho.

Misaada iliyotolewa ni pamoja na,chumvi katoni 1, unga wa ngano kilo 50,mchele kilo 100,unga wa sembe kilo 200,sukari kilo 20,mafuta ya kupikia lita 10 na sabuni za unga za kufulia kilo 30 vyote vikiwa na thamani ya shilingi 506,700/=.

Akikabidhi msaada huo wa chakula  kwa mkuu wa  kitengo cha Walemavu katika kituo cha Buhangija Jumuishi mwalimu  Bright Mduma mwandaaji wa shindano la Miss Shinyanga 2014 na Miss Talent Shinyanga 2014 bi Asela Magaka  kutoka Asela Promotions amesema ameamua kuwapeleka warembo hao katika kituo hicho ili wajue mambo yanaoendelea katika jamii ikizingatiwa kuwa kauli mbiu ni “Urembo, sanaa na jamii”.

“Tunao wajibu wa kujua namna jamii inavyoishi,urembo lazima uende sawa na jamii,nimewaleta washiriki wa miss Shinyanga 2014 ili wajue kuwa urembo unahusiano na mambo ya jamii,wajue jamii inahitaji nini,na umuhimu wa kusaidia jamii,hii itasaidia warembo hawa kuwa mabalozi wazuri katika kusaidia watu mbalimbali  wenye mahitaji maalum katika jamii”,aliongeza Magaka.

Katika hatua nyingine Magaka alieleza kukerwa na tabia ya baadhi ya watu katika jamii wanaoua watu wenye ulemavu kwa kuamini kuwa watapata utajiri na kuwataka waache vitendo hivyo kwani kwenda kinyume na haki za binadamu kwa sababu kila mtu ana haki ya kuishi na mwenye uwezo wa kutoa uhai wa binadamu ni mungu pekee.

Kwa upande wao washiriki wa shindano la Miss Shinyanga 2014 ambao baadhi yao walijikuta wakitokwa na machozi waliiomba serikali kuwachukulia sheria haraka iwezekanavyo wahusika wa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi badala ya kila mara kusema Uchunguzi unaendelea

Naye  mkuu wa kitengo cha walemavu kituo cha Buhangija mwalimu Bright Mduma amemshukuru mwandaaji wa shindano la mrembo wa mkoa wa Shinyanga 2014 kwa kuona umuhimu wa kusaidia watoto hao na kuwaomba washiriki wa shindano hilo kuwa mabalozi katika jamii kuhamasisha mashirika,taasisi na watu mbalimbali wenye mapenzi mema kujitokeza kuwasaidia watoto hao.

Aidha  Mduma amesema kituo cha kulelea watoto cha Buhangija cha mjini Shinyanga hivi sasa kinalea watoto 36 wasioona,48 wasiosikia na wenye ulemavu wa ngozi 180 huku changamoto ikiwa ni mabweni kwani sasa wanalazimika kulala watoto zaidi ya mmoja kitanda kimoja ambapo mabweni mawili yanahitajika kwa ajili ya watoto wa kiume na moja kwa watoto wa kike.

Kufuatia changamoto ya mabweni, warembo hao 20 wanaoshiriki  shindano la Miss Shinyanga 2014 wakiongozwa na mwandaaji wa Shindano hilo litakalofanyika terehe 28,Juni,2014 waliahidi kuchangia mifuko 18 ya saruji kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa bweni la wavulana lililoanza kujengwa 2013 na Miss Tanzania mwaka 2012 Brigette Alfred.

Jumla ya shilingi 80,000/= zilipatikana papo hapo na kukabidhiwa kwa mkuu wa kitengo cha walemavu mwalimu Bright Mduma,kwa ajili ya mifuko ya saruji miwili kati ya 18 waliyoahidi na kubakiza mifuko 16 katika ahadi yao kuchangia ujenzi wa bweni hilo.

Ziara ya washiriki wa shindano la mrembo wa mkoa wa Shinyanga 2014 imefanyika ikiwa wapo katika maandalizi ya shindano hilo litakalofanyika Juni 28,mwaka 2014 mjini Kahama ambapo kabla ya Shindano hilo kutafanyika shindano la kutafuta mrembo wa mkoa mwenye kipaji litakalofanyika Siku ya Jumatano Juni 25,2014 mjini Shinyanga.

Na Kadama Malunde-Malunde1 blog -Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post