CCM YACHANGANYWA TENA SHINYANGA,KATIBU MWENEZI WA CCM SHINYANGA MJINI AUNGA MKONO SERIKALI 3,KAMA MBUNGE WA KAHAMA

Katikati ni ndugu  Charles Shigino Katibu mwenezi wa CCM wilaya ya shinyanga mjini akiwa anahojiwa katika kipindi cha SAUTI YA WATU ndani ya studio ya Radio Faraja FM Stereo ya mjini Shinyanga ambapo katibu huyo anadai yeye binafsi anataka serikali 3 japo sera ya chama chake inataka serikali mbili(Picha na Veroca Natalisi)
Wakati mvutano wa serikali mbili,serikali tatu,ukiendelea kuchukua sura mpya kila kukicha,Katibu wa siasa na uenezi  CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Charles Shigino ameunga mkono muundo wa serikali tatu na kueleza kuwa hayo ndiyo maoni ya wananchi walio wengi yaliyopitishwa katika mchakato wa rasimu ya katiba ambayo iliundwa na tume ya Jaji Warioba.

Akizungumza jana jioni katika kipindi cha Sauti ya watu kinachorushwa na radio faraja Fm stereo inayomilikiwa na kanisa katoliki jimbo la Shinyanga, Shigino alisema suala linalosumbua na kuleta migogoro,migongano na matusi katika mchakato wa kuunda katiba mpya ni kutokana muingiliano wa  sera ya vyama.

Alisema hivi sasa kila chama kinakuwa na msimamo wake mfano CCM kina msimamo wa serikari mbili, CHADEMA, CUF kinataka serikari tatu, na kufuatia hali hiyo wafuasi wa vyama hivyo lazima wafuate msimamo wa vyama vyao suala ambalo linaleta mfarakano

Shigino alidai kuwa yeye binafsi anaunga mkono muundo wa Serikali tatu lakini kutokana na sera ya chama chake cha mapinduzi inamlazimu awe muumini wa Serikari mbili.

Akizungumzia kuhusu suala la Umoja wa katiba ya wananchi (UKAWA)  kutoka nje ya bunge na kususia vikao vya bunge la katiba linaoendelea mkoani Dodoma alidai kuwa wabunge hao wapo sawa kususia bunge hilo kwani asilimia kubwa ya wabunge waliobaki ndani ya bunge wamekuwa wakiwanyanyasa wabunge hao kwa kukejeri hoja zao na wakiwazomea kitendo ambacho amedai ni ukiukwaji wa haki na kanuni za bunge.

Shigino ameonesha msimamo wake wa kutaka serikali tatu,ikiwa ni siku chache tu baada ya mbunge wa Kahama James Lembeli kuonesha msimamo wake kuunga mkono serikali tatu hivyo kwenda kinyume na msimamo wa chama chao kinachotetea  na kuamini serikali mbili.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments